Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 18 | Sitting 8 | Community Development, Gender and Children | Maswali kwa Waziri Mkuu | 5 | 2025-02-06 |
Name
Martha Festo Mariki
Gender
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa wanawake ni kundi muhimu na kwa kuwa tunawategemea sana wanawake katika familia zetu na katika kizazi na endelevu na Taifa kwa ujumla na kwa kuwa wanawake wamekuwa wakipambana sana kujikwamua kiuchumi hasa katika maeneo yenye mfumo dume.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wanawake wanaendelea kupata ajira za kutosha sawa na makundi mengine ukilinganisha na ushindani wa ajira uliopo? (Makofi)
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kupigania haki za wanawake na hamu yake ya kuona fursa za akinamama zinapatikana. Wanawake ni kundi muhimu sana na Serikali imeendelea kuratibu shughuli mbalimbali zinazokuwa kuwawezesha akinamama kuweza kumudu kuboresha uchumi binafsi na kuendesha shughuli zao kama viongozi wa familia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili Mheshimiwa Mariki, amezungumzia Uchumi, lakini akazungumzia ushindani wa ajira, muhimu kwenye sekta ya ajira Waheshimiwa Wabunge tunajua kwamba Serikali ina ajira rasmi na ajira zisizokuwa rasmi, lakini ajira hizi zipo zile ambazo zinahitaji ujuzi maalum na hizi ndio ambazo zinazungumzwa sana kuwa na ushindani mkubwa na kundi lote linaweza likaachwa nyuma kutokana na kukosa sifa kadri ilivyotakiwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imeweka mpango mkakati wa kumwendeleza mwanamke. Moja, hata mabadiliko ya Sera ya Elimu ambayo sasa tunayo imetoa fursa ya wazi kwa wanawake au wasichana kupata elimu kuanzia ngazi ya awali mpaka vyuo vikuu, lakini pia umewekwa msisitizo maalum kwa ajili ya elimu, zile taaluma zenye ujuzi ili kumwezesha mwanamke kuingia kwenye shindani iwe ni wa ajira au katika kujitafutia uchumi binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili nalo tumejitahidi kuweka mifumo ambayo inamwezesha mwanamke kujiwezesha kupata uchumi. Tumefungua fursa ndani ya Serikali kupitia Mifuko mbalimbali kuwezesha kutoa mikopo na wanawake nao wanapata mikopo, lakini tumeweka pia Mfuko kwenye halmashauri zetu ambao tumetenga 10%, asilimia nne ni kwa ajili ya wanawake ambao pia wanaweza kwenda kukopa na haina ya riba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imezungumza na taasisi za fedha zihakikishe kuwa taasisi hizi zinafungua dirisha linalowezesha akinamama, vijana na makundi mengine kuweza kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi ili kumwezesha mwanamke au yeyote yule kati ya wakopaji kupata nafasi ya kuweza kuboresha uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia kwenye ajira sasa huku Serikali nayo inawaangalia sana wanawake pale ambapo panakuwa na ushindani wa mwanamke na mwanaume, lakini mwanamke anakuwa yupo kwenye ushindani ule basi nafasi ya kwanza anapewa mwanamke ili aweze kuingia kwenye hiyo.
Mheshimiwa Spika, haya ni malengo ya Serikali ya kufikia 50/50. Kwa hiyo, mikakati yote hii inaonesha dhamira ya wazi ya Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba mwanamke naye anapata nafasi ya kushiriki katika kukuza uchumi wa Taifa hili na kuchangia uchumi wa Taifa hili vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sera tuliyonayo ndani ya Serikali inaonesha jitihada za wazi kwa ajili ya kumhudumia mwanamke na kusimamia mwenendo wa shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, vilevile, ulinzi umeimarishwa pia na kuhakikisha kwamba anapata fursa ya kupata uwezo wa kuendesha shughuli yoyote ya kiuchumi wakati wowote anapoamua kufanya hivyo. Huo ndio mwelekeo wa Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved