Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 4 Sitting 3 Other Sectors Maswali kwa Waziri Mkuu 2 2016-09-08

Name

Jaku Hashim Ayoub

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Primary Question

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Nami nikushukuru na vilevile nikutakie afya njema na kila zito Mwenyezi Mungu afanye jepesi kwa upande wako.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali hii isingekuweko madarakani bila kuwepo wananchi na wananchi ndiyo Serikali na Serikali ni wananchi, hata Mheshimiwa Waziri Mkuu wewe mwenyewe bila kuweko wananchi usingepata Uwaziri Mkuu hata Mheshimiwa Rais pamoja na sisi Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani.
Mheshimiwa Spika, swali, afya huwezi kupata bila kupata chakula, mwanzo upate chakula ili upate afya. Hivi sasa kumekuwa na harufu inaweza ikawa nzuri au ni mbaya.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upungufu wa chakula ikiwemo bidhaa muhimu ya sukari, na sijui kama Serikali mmefanya utafiti gani kuliangalia suala hili. Msemo wa Waswahili husema, usipojenga ufa, hutajenga ukuta. Mmechukua jitihada gani kama Serikali kuangalia hali ya sukari na mchele ilivyo sasa? Na wanaoumia ni wananchi na ukizingatia kesho kutwa tuna sikukuu na inahitaji sukari kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Je, kuna harufu Serikali imeagiza sukari. Ni kweli suala hilo kwa ajili ya kuwajali wananchi wake?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ameeleza maneno mengi lakini muhimu ni kwamba kuna harufu ya upungufu wa bidhaa ya sukari nchini. Ni kweli huko nyuma tulikuwa na tatizo la sukari nchini kote na Serikali ikafanya jitihada ya kutambua mahitaji ya nchi, na yale mapungufu tuliyafanyia kazi kwa kuagiza sukari nje ya nchi na kuleta ndani kwa kiwango ambacho hakitaathiri uzalishaji wa ndani ili tuweze kuendelea kutoa huduma hiyo. Tumeendelea kufanya hilo mpaka pale ambapo tumeridhika kwamba viwanda vyetu vya ndani vimeanza kuzalisha na kuona uzalishaji ule na sukari ambayo tumeingiza vinaweza kutufikisha tena msimu ujao wa uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, suala la sukari hatujaishia tu kuwa na maazimio ya kuagiza toka nje. Mkakati mkubwa tuliofanya ni kuhakikisha tunaimarisha viwanda vya ndani viweze kuzalisha. Tumekutana na wazalishaji wote wa sukari, TPC, Kilombero, Kagera pamoja na Mtibwa kupata picha ya uzalishaji kwenye viwanda vyao na mkakati walionao kuendeleza uzalishaji. Lakini bado tumegundua kwamba viwanda vyetu havitakuwa na uwezo kwa kipindi cha miaka minne ijayo kuzalisha sukari ikatosheleza nchini. Lakini pia kumekuwa na wasiwasi wa takwimu za mahitaji ya sukari nchini kwa sababu nchi jirani ya Kenya yenye watu milioni 45 mahitaji ya sukari ni tani 800,000, lakini tathmini ya Idara yetu ya Kilimo nchini kwa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 45 ile ile wanatuambia takwimu zile zinahitaji tani 420,000; kwa hiyo utaona tuna upungufu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, tulichokifanya; kwanza tumeagiza Wizara ya Kilimo ifanye utafiti wa kina kuona mahitaji ya sukari nchini, lakini pili kutokana na maelezo tuliyopata kutoka kwa viwanda tumewapa maelekezo ya kuzalisha zaidi ili tuongeze sukari, na tumekubaliana hilo. Tatu, tumeamua kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda na uhamasishaji wa kilimo cha miwa ili tuweze kuzalisha sukari inayoweza kutosheleza mahitaji ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tayari tumeshapata wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza kwenye ulimaji wa miwa pamoja na uzalishaji wa sukari nchini ili na sisi tufikie kiwango ambacho kitakwenda kutambulika baada ya Wizara ya Kilimo kufanya sensa yake. Lakini wakati wote huu Serikali itahakikisha kwamba nchi haikosi sukari na wananchi wanaweza kupata kinywaji ambacho kinahitaji sukari, uendeshaji wa sukari kwenye viwanda kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayohitaji sukari ili tuweze kuhakikisha kwamba biashara hii na zao hili linatosheleza kwa matumizi ya ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia Mheshimiwa Jaku ametaka kuzungumzia upungufu wa chakula na jana Mheshimiwa Keissy aliomba Mwongozo wa kutaka maelezo ya hali ya chakula nchini na bado Serikali tumeahidi kutoa taarifa hapa Bungeni kabla ya mwisho wa wiki hii ya hali ya chakula nchini na mkakati wa taifa kama kuna upungufu huo wa kiasi hicho ili sasa kila mmoja wetu nchini aelewe nafasi tuliyonayo ili tuweze kushirikiana kwa pamoja kuondoa tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo taarifa ambayo itatolewa na Wizara ya Kilimo juu ya hali ya chakula ikiwemo na zao la sukari inaweza kusheheneza mahitaji ya uelewa kwenye eneo hili ahsante sana. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister

Name

Jaku Hashim Ayoub

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Question 1

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi niendelee kumshukuru Waziri Mkuu kwa umakini wake wa hali ya juu kujibu suala hili nililomuuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu hii imekuwa kama miongo ya mvua za masika. Ni sababu gani hasa Serikali kuwa haijajipanga kuonekana tatizo hili likafika pahala likamaliza kabisa suala la sukari?
Baada ya miezi mitatu, sita atakuja kiongozi mwingine atasahau kuhusu suala hili, kwa hiyo, Serikali ikajipange na suala hili, wananchi ndio muhimu na mlikuwa mkipiga kelele kuwa mtawajali wananchi, Serikali haiogopi hasara kwa ajili ya wananchi wake ni hilo tu Mheshimiwa.

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

SPIKA: Mimi naona kilichotolewa ni ushauri tu, lakini kwamba haijajipanga tusubiri ripoti ni ushauri tu.