Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 18 Sitting 13 Regional Administration and Local Government Authorities Maswali kwa Waziri Mkuu 3 2025-02-13

Name

Priscus Jacob Tarimo

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini zaidi kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya kwenye jamii yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza, Serikali ina mpango gani wa kuzipandisha hadhi Halmashari za Serikali za Mitaa ambazo zimeshapitia hatua zote za wilaya, mkoa ili zipandishwe hadhi?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa sasa upo uhitaji mkubwa wa baadhi ya maeneo ya kiutawala kutaka kupandishwa hadhi. Ninatambua pia Mheshimiwa Mbunge amekuwa akija mara kadhaa kuiomba Serikali kuupandisha hadhi ya Mji wa Moshi. Tunatambua zipo halmashauri kadhaa zimeshapitia hatua zote za kufikia vigezo vya kupata hadhi ya maeneo mapya ya utawala. Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa nyakati na kwa mara ya mwisho tulitoa maelekezo kwamba kwa sasa tutasimama kidogo kutoa maeneo mapya ya utawala baada ya kuwa tuna maeneo mapya ambayo sasa tunajenga miundombinu kuhakikisha kwamba rasilimali fedha na watu zinakamilika na maeneo haya kujiimarisha katika utoaji huduma kwa wananchi wa maeneo hayo mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pindi tutakapojiridhisha kwamba utoaji huduma kwenye maeneo haya miundombinu imekamika, rasilimali watu zinatosha, rasilimali fedha pale za kujiendesha ni nzuri tutaendelea kutoa vibali kwa maeneo mapya ili maeneo yale yote yenye uhitaji wa mamlaka mpya iweze kupata mamlaka hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa hiyo ninaamini Mji wa Moshi tayari umeshaleta taarifa, halmashauri wanaendelea kuchakata na kuona ukamilishaji wa miundombinu kwenye maeneo mapya ukoje na baadaye tutapata taarifa na Mheshimiwa Tarimo akiwa ni mmoja wa watu ambao wamehitaji sana mabadiliko kwenye mji wake basi Wizara yetu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI italishughulikia jambo hilo kulingana na wakati na kukamilika kwa mahitaji hayo. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister