Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 18 Sitting 13 Information, Culture, Arts and Sports Maswali kwa Waziri Mkuu 5 2025-02-13

Name

Nicholaus George Ngassa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Primary Question

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi kupata nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa nchini kwetu sekta ya michezo imekuwa ikikua kwa kasi sana na hili limedhihirishwa kutokana na kiwango cha soka nchini ambacho kimekua. Hata ukiangalia ligi yetu kwa sasa katika viwango vya Afrika tupo ndani ya ligi bora tano. Hili huwezi kulitengenisha na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza sekta ya michezo. Tumpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwa jemedari namba moja katika kuhakikisha sekta ya michezo inakua nchini kwa kujenga miundombinu ya michezo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ya Awamu ya Sita imetengeneza mazingira mazuri ambayo yamevutia wawekezaji na wadau mbalimbali kushiriki katika sekta hii. Swali langu Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, ni ipi mikakati madhubuti ya Serikali ambayo itachukuliwa katika kuhakikisha halmashauri zetu kupitia mapato ya ndani wanajenga viwanja mbalimbali vya michezo vinavyokidhi vigezo vya kitaifa katika kukuza sekta hii ya michezo?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Ngassa, Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, upo ukweli kwamba kiwango cha michezo nchini kimepanda na ninataka nitumie nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yeye mwenyewe amekuwa nambari moja kuhamasisha Watanzania kushikiri katika michezo mbalimbali. Tumeendelea kufanya maboresho ya maeneo ya kufanyia mazoezi ikiwemo na viwanja na zipo halmashauri kadhaa ambazo zimeendelea kutenga bajeti zao kwa ajili ya kujenga viwanja na huku Serikali Kuu pia tukijenga viwanja vyenye viwango vya kimataifa kwa lengo la kuwafanya Watanzania wanapofanya mazoezi wafanye mazoezi kwenye viwanja vyenye viwango vya kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukua mfano wa mpira wa miguu huu umetuletea heshima nchi yetu. Kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba mpira wa miguu leo Tanzania ndio wenye ligi bora Barani Afrika. Sasa tumeona timu yetu ya Taifa, ligi yetu imepanda viwango mpaka nafasi ya nne Barani Afrika. Nimeona pia hata kwenye ITV kila siku inaeleza na kidunia ninadhani tupo wa 57, tunaona kwenye TV Azam wanatangaza mafanikio hayo kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio haya nayatokana pia na ujenzi wa viwanja kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye halmashari ambazo Mheshimiwa Mbunge amesema wanatengeneza kwa fedha zao kama vile Bukoba pale Kaitaba wamejenga uwanja mzuri, Nyamagana Jiji la Mwanza wamejenga uwanja mzuri. Pia tumeona kule Wilayani Ruangwa napo wamejenga uwanja mzuri, Kinondoni (KMC) wamejenga uwanja mzuri na sasa hivi Chunya napo wanajenga uwanja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo zipo jitihada za kila halmashauri kujenga viwanja vyenye viwango vya kimataifa na ndivyo vinapandisha hadhi ya kiwango cha soka nchini. Hata kwa vilabu kimoja kimoja tumeona na ninyi ni mashahidi, timu zetu zile kongwe mbili Simba ni ya saba kwenye ngazi ya CAF na Yanga ni ya 13, Simba ya saba kwenye CAF na Yanga ya 13. Vyote hivi vipo zaidi ndani ya 20 bora, vinatuletea heshima kubwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya michezo nchini kwa michezo yote ili kuhakikisha Watanzania wanapata kushiriki kwenye viwanja vilivyo bora, maeneo yenye miundombinu iliyo bora kwa lengo la kuwawezesha kufanya mazoezi kwenye viwanja hivyo. Tutaendelea kuimarisha ufundi katika michezo hiyo ili pia viwango viendelee kupanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa halmashauri na mikoa kuhakikisha kwamba taasisi zetu zote, maeneo yetu yote ya umma vijijini, wilayani na mikoani tunakuwa na viwanja bora vya kuwawezesha wananchi kushiriki kwenye michezo yao. Pale ambapo tuna viwanja tutahakikisha kwamba tunaviimarisha na kuviongezea uwezo wa viwanja hivyo kuweza kupokea washiriki wengi wa michezo kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutahakikisha kuwa ujenzi wa viwanja unaendelea na kwa ngazi ya Taifa mnajua kwamba sasa hivi tunajenga uwanja mkubwa Arusha, lakini pia tutakarabati uwanja wa Benjamin Mkapa, uwanja wa Uhuru na kule Zanzibar viwanja vya Gombani na Amani vinaimarishwa. Malengo ni kutaka kukaribisha heshima tuliyopewa ya kuweza kuwa wenyeji wa mashindano ya CHAN mwezi wa nane mwaka huu, na tunao uwezo huo. Pia mashindano ya AFCON mwaka 2027, uwezo huo tunao. Hiyo ndiyo faraja ya Watanzania kuona kwamba mashirikisho mbalimbali ya michezo duniani yanaiona Tanzania kuwa ni sehemu sahihi ya kuendesha michezo hiyo kwa ngazi ya Afrika na ya dunia pia. Huo ndiyo mkakati wetu wa Serikali, ahsante. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister