Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 14 | Sitting 1 | East African Co-operation and International Affairs | Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki | 16 | 2024-01-30 |
Name
Abdullah Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mahonda
Primary Question
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI aliuliza:-
Je, nini maana ya non-aligned katika msimamo wa Tanzania Kimataifa wa kutofungamana?
Name
Amber. Mbarouk Nassor Mbarouk
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdullah Ali Mwinyi, Mbunge wa Mahonda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, non-aligned ina maana ya kutofungamana ama kushikamana, kiitikadi na kimsimamo na nchi ama kundi la nchi zenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani. Dhana hii ilikuja mara tu baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya dunia mwaka 1945, ambapo dunia ilishuhudia kuibuka kwa kambi mbili zilizokuwa zinahasimiana ambazo ni Marekani na washirika wake chini ya mwamvuli wa NATO na uliokuwa Umoja wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR) na washirika wake chini ya mwamvuli wa Warsaw Pact.
Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, nchi ambazo ziliamini kutofungamana ama kuambatana na upande wowote zilianzisha Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Aligned Movement - NAM). Tanzania ilijiunga na umoja huu mwaka 1961 mara tu baada ya uhuru. Dhana ya kutofungamana na upande wowote ni miongoni mwa misingi ya sera yetu ya mambo ya nje.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Tanzania imeendelea kuwa mwanachama wa NAM kwa kutekeleza misingi ya kutofungamana na upande wowote katika maamuzi mbalimbali ambayo yanachukuliwa kwenye ajenda za kimataifa kwa kuzingatia uhuru na mipaka ya nchi (sovereignty and territorial integrity), kupinga matumizi ya nguvu za kijeshi, haki na usawa duniani na maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved