Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 35 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 292 2016-06-02

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Primary Question

MHE. DOTO M. BITEKO aliuliza:-
Maafisa wa Idara ya Misitu walivamia wananchi wa kitongoji cha Idosero kilichosajiliwa kwa GN na kuchoma nyumba 40 za wananchi na kuharibu mazao yao.
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Idosero kwa hasara kubwa waliyopata?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko, Mbunge wa Jimbo la Bukombe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Idosero limo ndani ya misitu ya Biharamulo na Kahama yenye jumla ya hekta 134,684 iliyoanzishwa kwa sheria, Sura ya 389, Nyongeza ya 59 ya mwaka 1954 na kufanyiwa marekebisho kwa Tangazo la Serikali namba 311 la mwaka 1959. Misitu hii kwa sasa inasimamiwa na Sheria ya Misitu Sura ya 323 Toleo la mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 07 Novemba, 2015 Maafisa kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe walifanya operesheni ya kuhamisha wavamizi katika misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakazi wa eneo la Idosero walianza kuingia na kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya misitu hii mwaka 1985 na uvamizi uliongezeka hatua kwa hatua na kukithiri baada ya kutolewa kwa Tangazo la Serikali Namba 221 la tarehe 27 Juni, 2015 lililolipa eneo hilo hadhi ya kitongoji kipya katika kijiji cha Nampalahala, bila kubainisha mipaka ya kitongoji hicho. Tamko hilo lilikizana na matangazo ya Serikali yaliyopita au yaliyotangulia na Sheria ya Misitu Sura ya 323 ya mwaka 2002 yanayotambua kuwa eneo hilo ni hifadhi ya misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama yaWilaya ya Bukombe ilifanya mkutano na wakazi wa eneo la Idosero tarehe 08 Mei, 2015 na kuwataka waondoke kwa hiari yao ifikapo tarehe 08 Julai, 2015. Wakazi hao walikaidi amri hiyo kwa madai kuwa eneo hilo si hifadhi kwa kuwa Tangazo la Serikali Namba 221 limetambua eneo hilo kuwa ni kitongoji cha makazi. Aidha, mnamo tarehe 09 hadi 20 Juni, 2014 Serikali ilifanya sensa ya kuhesabu watu na kubaini kuwepo kwa kaya 309 zenye jumla ya wakazi 2,777 ndani ya eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Sheria ya Misitu Sura ya 323 ya mwaka 2002, watumishi wa TFS au Mamlaka ya Misitu walifanya zoezi la kuwaondoa wavamizi katika eneo hilo ambalo hata hivyo halifanikiwa na wananchi bado wanaendelea kuhamia na kupanua shughuli za kibinadamu katika misitu hiyo na kuendelea kufanya uharibifu wenye athari kubwa za kimazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishaeleza katika majibu ya msingi na nyongeza yaliyopita kwa maeneo yenye changamoto zinazofanana na hii utatuzi wa mgogoro huu utapatikana wakati wa zoezi la pamoja la utatuzi wa matatizo ya ardhi linalotarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa shughuli za Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja.