Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 15 Sitting 46 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Kilimo 600 2024-06-12

Name

Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, lini kongani za korosho za Maranje Nanyamba zitajengwa ikiwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Mtwara?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Korosho imeanza kutekeleza Mradi wa Kongani ya Viwanda vya Kubangua Korosho katika Kijiji cha Maranje Mkoani Mtwara. Kongani ya Korosho ya Maranje - Nanyamba ni mradi wa kimkakati unaolenga kuongeza thamani ya korosho, kuongeza kipato cha mkulima kwa kuuza korosho zilizoongezwa thamani badala ya kuuza korosho ghafi pamoja na kuongeza ajira katika mnyororo wa uzalishaji wa korosho na mazao yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 10 Juni, 2024 uthamini wa eneo la mradi ekari 1,572 umekamilika ikiwa ni pamoja na ulipaji wa fidia kwa wananchi. Aidha, Serikali imetoa fedha shilingi bilioni 7.5 kwa Bodi ya Korosho kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika eneo la ekari 354 kati ya ekari 1,572. Shughuli zilizofanyika mpaka sasa ni kusafisha eneo hilo pamoja na kuanza kwa shughuli za uchimbaji wa visima vya maji na kupeleka umeme katika eneo hilo. Aidha, mkandarasi tayari ameshapatikana kwa ajili ya kutengeneza barabara za ndani kwa kiwango cha changarawe, pamoja na kujenga maghala mawili ya mfano na kiwanda cha kubangua korosho katika eneo hilo. Serikali kupitia Bodi ya Korosho tayari imeanza kuongea na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujenga viwanda vya kuongeza thamani korosho katika eneo hilo.