Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 15 | Sitting 26 | Lands, Housing and Human Settlement Development | Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi | 349 | 2024-05-15 |
Name
Bahati Keneth Ndingo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Primary Question
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanga matumizi bora ya ardhi kutokana na kasi ya ongezeko la watu nchini?
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali hili naomba kwanza niombe radhi, kwamba Mheshimiwa aliyeuliza swali ni Mbunge wa Mbarali na si Mbunge wa Viti Maalum. Naomba hiyo iingie kwenye Hansard.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, jumla ya vijiji 4,024 kati ya vijiji 12,318 vilivyopo nchini vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Miongoni mwa mikakati inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na kuzihimiza mamlaka za upangaji kutenga fedha kwa ajili ya uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, kuendelea kutenga bajeti kwa Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, kuandaa, kuwezesha na kusimamia upangaji wa matumizi ya ardhi, kuhamasisha wadau kuchangia upangaji wa matumizi ya ardhi na kubuni miradi ambayo inawezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilibuni na kutekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki (LTIP), ambao umelenga kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi miradi 1,667 katika kipindi cha miaka mitano. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imetenga jumla ya shilingi 5,041,232,000 kwa ajili ya kuiwezesha Tume kuendelea kupanga matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Mbarali na maeneo mengine ya nchi kuwa azma ya Serikali ni kupanga miji na vijiji vyote ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya ardhi linalochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la watu. Niendelee kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge, kuhakikisha kwamba halmashauri zao zinaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kupanga miji na kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved