Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 15 Sitting 30 Works and Transport Wizara ya Ujenzi 397 2024-05-21

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Primary Question

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, upi ukomo wa kuweka alama za upana wa Barabara Vijijini na kuwataka Wananchi kubomoa nyumba kutumia Sheria ya Mwaka 1932 na 2007?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na Sheria ya Barabara Na. 40 ya Mwaka 1932, hifadhi ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS ilikuwa mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande isipokuwa kwa barabara ya Morogoro ambao hifadhi yake ilikuwa kati ya mita 22.5 hadi 121.9 kuanzia Dar es Salaam City Hall hadi Daraja la Ruvu. TANROADS imeweka alama ya ‘X’ ya rangi nyekundu kwa mali za wananchi zilizopo ndani ya mita 22.5 na kuwataka wananchi waondoe mali hizo kwa gharama zao wenyewe kwa kuwa wamevamia eneo la hifadhi ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 iliongeza hifadhi ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS kutoka mita 22.5 kuwa mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande. Katika kutekeleza Sheria hii, TANROADS imeweka alama ya ‘X’ za rangi ya kijani kuonesha eneo la mita 7.5 liliongezeka kila upande ambapo wananchi waliopo katika eneo hili hawapaswi kuondoa mali zao mpaka watakapolipwa fidia.