Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 15 | Sitting 54 | Planning and Investment | Ofisi ya Rais: Mipango na Uwekezaji | 694 | 2024-06-26 |
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kunakuwa na mpango wa maendeleo walau wa miaka 50 pamoja na kuwa na vipaumbele vya Taifa?
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kutoa majibu kwa upande wa Serikali, naomba uniruhusu kwa dakika moja nitoe maneno yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, cha kwanza kabisa namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na mpaka leo tuko hapa, lakini nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniteua katika nafasi hii kumsaidia katika ofisi yake na hasa katika kusimamia masuala ya mipango na uwekezaji, lingine nikushukuru sana, maana malezi yako yamenifanya niwe hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho niendelee kuwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Maswa Mashariki kwa sababu nao ndiyo wamenifanya niweze kufika hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, basi sasa kwa niaba ya Waziri wangu wa Mipango na Uwekezaji naomba nijibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ajenda ya maendeleo ya Taifa letu inaongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambapo utekelezaji wake umegawanyika katika mipango ya maendeleo ya muda wa kati na muda mfupi, vilevile inaainisha vipaumbele vyake. Utekelezaji wa Dira ya mwaka 2020/2025 unatarajiwa kufikia ukomo wake mwezi Juni, 2026.
Mheshimiwa Spika, msingi wa kuwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya kipindi cha miaka 25 unajengwa katika sababu kuu mbili; kwanza, ni wastani wa idadi ya miaka ya kizazi kimoja (single generation) kipindi cha Dira ya Taifa ya Maendeleo kwa kiasi kikubwa kinawiana na wastani wa umri wa kizazi kimoja (single generation) ambapo ni kati ya miaka 20 hadi 30 na sababu ya pili, ni uzoefu wa vipindi vya dira ya maendeleo katika nchi mbalimbali ambapo tathmini ya dira za nchi 18 za Afrika na Asia zinazoonesha kuwa wastani wa kipindi cha Dira ya Taifa ya Maendeleo ni miaka 21.
Mheshimiwa Spika, kipindi husika kinaonekana kinatoa fursa ya kuainisha utekelezaji wa mikakati mahususi ya kufikia malengo ya dira pasipo kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko au sababu zilizo nje ya uwezo na wa udhibiti wa nchi husika kwa mfano teknolojia, siasa za kijografia (geo-politics) na kadhalika.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved