Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 19 | Sitting 2 | Good Governance | Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) | 20 | 2025-04-09 |
Name
Zahor Mohamed Haji
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Primary Question
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kupambana na rushwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ikizingatia kuna upungufu wa Watumishi pamoja na vitendea kazi?
Name
George Boniface Simbachawene
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibakwe
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga na kudhamiria kuwa na uchaguzi huru na wa haki ambao viongozi watachaguliwa kutokana na uwezo wao wa kuwaongoza na kuwahudumia wananchi na sio kwa kuwarubuni wapiga kura kwa rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza azma hii ya Serikali, TAKUKURU imejipanga kudhibiti na kuzuia rushwa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kutoa elimu kwa umma kwa kutumia njia mbalimbali kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi, kufuatilia nyendo za wagombea na wapambe wao kwa lengo la kuzuia vitendo vya rushwa, kukusanya taarifa za kiintelijensia kuhusu vyanzo vya mapato ya wagombea, wapambe na vyama vya siasa ili kudhibiti matumizi ya fedha haramu, kuchunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wagombea na wapambe watakaojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2023/2024, Serikali iliiwezesha TAKUKURU kuajiri watumishi 350, kununua magari 178 na vitendeakazi vingine ili kuimarisha utendaji kazi katika ngazi ya mikoa na wilaya. Serikali itaendelea kuiwezesha TAKUKURU kwa watumishi, fedha na vitendeakazi ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa hapa nchini.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved