Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 19 Sitting 39 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 504 2025-06-04

Name

Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Primary Question

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, jitihada gani zimefanyika kurahisisha upatikanaji wa visa kwa watalii wenye uraia tofauti wanaokuja nchini kwa mwitikio wa Royal Tour?

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha utaratibu wa utoaji wa visa nchini ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani. Mathalani, Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imeanzisha mfumo wa maombi ya visa kwa njia ya mtandao unaowawezesha watalii kuomba visa popote walipo duniani bila kulazimika kufika ubalozini. Halikadhalika, Serikali imeboresha Kanuni za Uhamiaji za mwaka 2023 ambapo kwa sasa watalii wanaotumia visitors pass wanaruhusiwa kutembelea nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kurejea Tanzania bila hitaji la kuomba upya pasi ya kuingia nchini alimradi pasi aliyopewa iwe haijaisha muda wake.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Serikali imeendelea kuingia makubaliano na nchi mbalimbali ili kurahisisha utaratibu wa visa ambapo kwa sasa raia wa nchi 71 hawahitaji visa wanapoingia nchini. Aidha, kwa sasa watalii kutoka katika mataifa mengi duniani wanaruhusiwa kupata visa wanapowasili kwenye viwanja vya ndege vya kimataifa kama Julius Nyerere, Kilimanjaro na Zanzibar. Vilevile, Serikali imefanya mapitio ya nchi zilizo kwenye kundi la visa rejea kwa lengo la kufanya maboresho.