Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 4 | Sitting 8 | Energy and Minerals | Wizara ya Nishat | 108 | 2016-09-16 |
Name
Willy Qulwi Qambalo
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Karatu
Primary Question
MHE. WILLY Q. QAMBALO aliuliza:-
Katika kupunguza tatizo sugu la maji Wilaya ya Karatu baadhi ya vijiji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamechimba visima virefu 12 katika maeneo ya Basodawish, Endabash, Rhotia Kainani, Endamarariek, Getamock, Karatu Mjini, Gongali na kadhalika, visima hivyo vinaendeshwa kwa kutumia mashine za dizeli jambo ambalo linasababisha gharama kubwa za uendeshaji.
Je, Serikali itawasidia lini wananchi hao kwa kuwaunganisha na nishati ya umeme katika visima hivyo ili kupunguza gharama za uendeshaji?
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kabla sijatoa maelezo ya kuhusiana na swali la Mheshimiwa Mbunge niombe kwa ridhaa ya kiti chako Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge nichukue nafasi moja ya kuwapa pole sana wananchi wa Jimbo langu Chato kwa kupata msiba mkubwa ambao umetokea juzi baada mvua kubwa kunyesha kwenye Jimbo la Chato na kusababisha wananchi wawili kupoteza maisha yao na wananchi wengine 17 kujeruhiwa vibaya sana. Kwa heshima ya kiti chako basi kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge tujumuike na wananchi wa Chato katika kuomboleza msiba huo mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sasa kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Willy Qulwi Qambalo, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kufikisha umeme katika maeneo yote nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Wilaya ya Karatu. Kipaumbele katika kutekeleza miradi ya umeme ni pamoja na kufikisha umeme katika miundombinu inayotoa huduma za kijamii ikijumuisha visima vya maji, shule, zahanati, makanisa, misikiti na maeneo ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Basodawish, Endabash, Endamarariek, Getamock pamoja na maeneo ya Karatu Mjini yamefikishiwa huduma ya umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Pili. Hata hivyo huduma ya umeme haijafikishwa katika visima vya maji vilivyopo katika maeneo niliyoyataja. Kazi ya kupeleka umeme katika visima hivyo itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 12.6 na ufugaji wa transfoma tano za KVA 100 kila moja. Gharama ya kazi hizi ni shilingi milioni 467.16. Visima vyote katika vijiji vilivyotajwa hapo juu vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika kisima kilichopo Karatu Mjini inahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 1.2 na kufunga transfoma ya ukubwa wa KVA100. Gharama ya kazi hii ni shilingi milioni 33.81 kazi imepangwa kutekelezwa kupitia bajeti ya TANESCO ya mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha vijiji vya Gongali, Gyekrum Lambo, Kainam Rhotia na Kambi Faru vitapata umeme kupitia mradi wa REA awamu ya Tatu. Kazi za kuvipatia umeme vijiji hivi itahusisha pia upelekaji umeme kwenye visima vya maji vilivyopo katika vijiji hivyo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved