Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 6 Sitting 2 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 27 2017-02-01

Name

Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Primary Question

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
Sheria zinatoa ridhaa kwa watu kuwinda ndani ya hifadhi:-
Je, Serikali inachukua hatua gani kutoa ridhaa kwa wananchi waishio maeneo ya hifadhi kupata ruhusa kisheria ili kuweza kuvua samaki ndani ya mabwawa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwa wanakijiji waishio maeneo ya hifadhi hususan Kata za Mwaseni, Mloka na nyingine?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka, Ngoroko na Kipungila Wilayani Rufiji waliruhusiwa kuingia ndani ya Pori la Akiba Selous na kuvua samaki. Hata hivyo, baadhi ya wanavijiji walikiuka taratibu zilizokuwa zimewekwa kwa kuingia ndani ya hifadhi bila kujiandikisha na kuvua samaki kinyume cha sheria. Aidha, baadhi yao walibainika kujihusisha na vitendo vya ujangili wa wanyamapori kama vile utoaji wa taarifa za mwenendo wa doria na uwindaji wa wanyamapori, uvuvi haramu wa kutumia sumu, ukataji miti ovyo kwa ajili ya kukaushia samaki na kutengeneza mitumbwi na uharibifu wa mazingira kutokana na uchomaji wa moto ovyo kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hali ya usalama katika maeneo ya uhifadhi ya wanyamapori, kwa sasa Wizara yangu itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba Selous. Hata hivyo, Wizara yangu inawashauri wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka na nyinginezo zilizo jirani kutumia mabwawa mengineyo yaliyopo nje ya pori yenye fursa kubwa ya kufanya shughuli za uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mabwawa hayo ni Zumbi katika Vijiji vya Nyaminywili, Kipugira na Kipo, Bwawa la Ruwe karibu na Mkongo, Bwawa la Lugongo katika Kijiji cha Mtanza na Bwawa la Zimbwini katika Mji wa Kibiti.
Mabwawa hayo na Mto Rufiji vinatoa fursa ya shughuli za uvuvi, hivyo kusaidia kuinua kipato cha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mahitaji ya wananchi katika maeneo haya, ya kufanya kazi na kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Wizara yangu inaendelea kushauriana na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kuhusu namna ya kutekeleza mpango wa kuwajengea mabwawa ya samaki ili pamoja na mabwawa ya asili yaliyopo yawawezeshe kufanya shughuli za uvuvi endelevu.