Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 6 | Sitting 3 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 38 | 2017-02-02 |
Name
Hawa Mchafu Chakoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA M. CHAKOMA, aliuliza:-
Tarehe 25 Oktoba, 2016 Kituo cha Televisheni cha Mlimani TV kilirusha Kipindi cha Urithi Wetu kilichozungumzia Malikale za Taifa letu na namna ambavyo agizo la Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete la ufunguzi wa nyayo za Laetoli linavyosuasua kutekelezwa kwa kisingizo cha ukosefu wa wataalam.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuajiri wataalam hao?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nyayo za Laetoli zilizogunduliwa na mtafiti Dkt. Mary Leakey mwaka 1978 katika eneo la Laetoli katika Hifadhi ya Ngorongoro ni ushahidi wa pekee duniani usiopingika kwamba binadamu wa umri wa miaka milioni 3.6 iliyopita waliweza kutembea wima kwa miguu miwili katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2007 aliagiza Wizara yangu kufukua nyayo hizo na kuzihifadhi kwa njia ya kisasa itakayoruhusu matumizi ya elimu na utalii kwa Watanzania na wageni na kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro igharamie kazi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unakadiriwa kugharimu takribani Dola za Marekani milioni 50 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 105. Fedha hizo zitatumika kuwasomesha wataalam, kuandaa michoro ya ujenzi wa makumbusho, kufukua na kuhifadhi nyayo, kusimamia ujenzi na kuweka mifumo ya uhifadhi. Fedha hizo ni nyingi ukilinganisha na mapato na majukumu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Hivyo Wizara yangu inaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kugharamia utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba hakuna hali ya kusuasua katika katika utekelezaji wa mradi huu muhimu na kwamba baadhi ya kazi zimekwishakamilika na nyingine ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zilizokamilika ni pamoja na kuundwa kwa Idara ya Urithi wa Utamaduni, kukamilika kwa michoro ya awali ya jengo la mapokezi, jengo la utafiti na jengo la elimu kwa umma, kuwasilishwa kwa tathmini ya athari kwa mazingira kwa mamlaka husika ikiwa ni pamoja na UNESCO kwa uchambuzi wa kina kwa lengo la kutoa idhini na mafunzo ya shahada ya uzamivu kwa watumishi wawili.
Kazi ambazo zinaendelea kutekelezwa ni pamoja na kukamilisha taratibu za ajira kwa baadhi ya wataalam wanaopatikana nchini na ukusanyaji wa takwimu sahihi kuhusu mazingira rafiki ya nyayo hizo kazi ambayo inafanywa na wataalam kutoka nje ya nchi na inatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2017 na kwa maana hiyo, napenda kusema kwamba kazi hii imekwishakamilika kwa sababu tulikuwa tumepanga ikamilike mwezi huu, mwaka 2017.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved