Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 6 | Sitting 7 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 77 | 2017-02-07 |
Name
Bonnah Ladislaus Kamoli
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Primary Question
MHE. BONNAH M. KALUWA aliuliza:-
Katika maeneo ya Kata mpya ya Bonyokwa Jimboni Segerea kuna msitu
unaoitwa “Msitu wa Nyuki” ambao kwa muda mrefu umekuwa kichaka cha
kujifichia majambazi; na wapo wananchi ndani ya Jimbo hilo waliokumbwa na
tatizo la bomoa bomoa katika Kata za Buguruni Mnyamani, Tabata Liwiti,
Vingunguti na Kipawa wanaozunguka bonde la Mto Msimbazi ambao hawana
pa kwenda:-
Je, Serikali haioni kuwa ni busara kurudisha Msitu huu kwa wananchi hao
waliokumbwa na tatizo la bomoabomoa ili waweze kuweka makazi yao eneo
hilo.
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii,
naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Moses Kaluwa, Mbunge wa
Segerea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Msitu wa Kinyerezi wenye ukubwa wa hekta 4.4
ulipimwa mwaka 1997 ukiwa chini ya usimamizi wa Serikali Kuu kwa kushirikiana
na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala. Msitu huu ambao ndio msitu pekee uliopo
ndani ya Jiji la Dar es Salaam ukiacha misitu ya mikoko, kwa sasa unatumika
kama Ukanda wa Kijani (Green belt), hifadhi ya ardhi kwa ajili ya kuzuia
mmomonyoko wa udongo ambao unatishia kutokea katika maeneo
yanayozunguka msitu na kituo kwa ajili ya mafunzo ya elimu ya misitu na
upandaji miti.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa msitu huu ndani ya Jiji ni fursa adimu
inayoweza kuendelezwa na kutumika kama sehemu muhimu ya kutembelea
kwa utalii katika Jiji la Dar es Salaam. Serikali ina mpango kabambe wa kufanya
msitu huu kuwa forest park ili kufanya shughuli za utalii wa kiikolojia (eco-tourism)
kwa kuwa katika msitu huo pamoja na sifa nyingine kuna aina za miti zilizo
hatarini kutoweka duniani ukiwemo mpingo. Hivyo, Serikali inahamasisha uhifadhi
shirikishi kwenye rasilimali hiyo kwa manufaa ya wananchi waishio jirani na msitu
huo na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la wananchi waliokumbwa na
zoezi la bomoa bomoa katika Kata za Buguruni Mnyamani, Tabata Liwiti,
Vingunguti na Kipawa wanaozunguka bonde la Mto Msimbazi na kukosa makazi,
Wizara yangu inawashauri wachukue hatua sahihi kwa kushirikiana na taasisi na
mamlaka husika za Serikali ili kupata elimu na taratibu za mipango miji
zitakazowezesha upatikanaji wa suluhisho endelevu la changamoto walizonazo
kuhusu makazi bila kuathiri dhana nzima ya uhifadhi endelevu wa misitu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved