Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 2 | Sitting 8 | Energy and Minerals | Wizara ya Nishat | 101 | 2016-02-04 |
Name
Kiswaga Boniventura Destery
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Primary Question
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Serikali imeweka mpango wa umeme vijijini ambapo kwa Jimbo la Magu ni asilimia 20 tu ya vijiji ndivyo vimepata umeme ambalo ni hitaji muhimu kwa kila Mtanzania:-
(a) Je, asilimia 80 ya vijiji vilivyobaki vitapata lini umeme?
(b) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la kukatikakatika kwa umeme nchini?
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Desdery Kiswaga, Mbunge wa Magu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua juhudi za Serikali za kusambaza umeme katika Jimbo lake la Magu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji 39 kati ya 142 vilivyoko kwenye Jimbo la Mheshimiwa sawa na 27% tayari vimepatiwa umeme. Hata hivyo, vijiji 18 sawa na 13% viko katika utekelezaji wa awamu ya pili na hivyo kufanya jumla ya vijiji 57% sawa na 40% kuwa vimepatiwa umeme mara baada ya awamu ya pili kukamilika Juni, 2016. Vijiji 34 kati ya 85 vilivyosalia vitajumuishwa kwenye mpango wa usambazaji umeme awamu ya tatu utakaoanza Juni, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kukatikakatika kwa umeme nchini inatokana na sababu za uchakavu na kuzidiwa kwa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme na vituo vya kupoza umeme. Sababu nyingine ni pamoja na matukio ya kulipuka kwa transfoma yanayosababishwa na radi hasa kipindi cha mvua pamoja na wizi wa mafuta ya transfoma unaofanywa na wananchi wasiokuwa waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na tatizo la kukatikakatika kwa umeme nchini, TANESCO inachukua hatua za kujenga mifumo ya njia kubwa za umeme wa msongo wa kilovoti 400 za backbone unaoanzia Iringa – Dodoma - Singida - Shinyanga. Kadhalika kuanzisha mradi wa North East Grid unaoanzia Dar es Salaam – Chalinze - Tanga - Arusha. Sambamba na miradi hiyo, upo mradi wa North West Grid unaoanzia Geita – Chalinze – Katavi – Kigoma - Rukwa - Mbeya. Hali kadhalika na mradi wa Makambako - Songea wenye kilovoti 220.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa miradi hii, kutaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo mengi nchini. TANESCO inakamilisha upanuzi wa mifumo ya usambazaji wa umeme katika Majiji makubwa ya Arusha, Dar es Salaam pamoja na Mwanza. Kazi zinazohusika ni pamoja na ujenzi wa njia mpya za umeme na kupanua vituo vya kupoza umeme (substations). Kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA Mkoani Kilimanjaro kutaimarisha sana upatikanaji wa umeme maeneo ya Mererani pamoja na uwanja wa ndege wa KIA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya kupoza umeme katika Jiji la Dar es Salaam vya Gongolamboto, Kipawa, Mbagala na Kurasini vitaunganishwa kwa njia ya sakiti mizunguko (ring circuits) kutoka Ubungo, Kinyerezi kuanzia Machi, 2016. Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo yanayohudumiwa na vituo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ni ule wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katikati ya Jiji la Dar es Salaam ukijumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 chini ya ardhi kwenda kituo cha Sokoine pamoja Kariakoo. Aidha, ifikapo Machi, 2016, TANESCO itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Udhibiti wa Mfumo wa Usambazaji wa Umeme kwa Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Distribution Management System).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo la umeme hasa kuungua kwa transfoma, TANESCO imeendelea kufunga mifumo ya kudhibiti radi (lightning arrestors) nchi nzima na kuachana na transfoma za mafuta hasa maeneo yaliyokithiri kwa wizi wa mafuta.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved