Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 25 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 205 2017-05-15

Name

Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Gereza la Kingulungundwa lililopo Wilayani Lindi linakabiliwa na uhaba mkubwa wa Nyumba za Askari na miundombinu mibovu:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha makazi ya Askari katika Gereza hilo?
(b) Gereza hili lipo umbali wa kilometa tatu kutoka barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda Lindi, lakini wakati wa masika, barabara hiyo haipitiki kwa gari kutokana na kujaa tope na maji. Je, Serikali haioni kuwa kukosekana kwa mawasiliano ya barabara kutoka Gerezani ni jambo la hatari?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la uchakavu na upungufu wa nyumba za Askari wa Jeshi la Magereza nchini na hali hiyo inatokana na baadhi ya nyumba kujengwa kabla ya uhuru ama katika maeneo mengine ambapo zilijengwa kwa matumizi ya muda wakati ikisubiri ujenzi wa nyumba za kudumu na za kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya nyumba za Askari Magereza hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni nyumba 4,221, hivyo kuwepo kwa upungufu wa nyumba 10,279 ambao unasababisha baadhi ya Askari kuishi nje ya Kambi. Kwa sasa Serikali ina mpango wa kuwajengea Askari Magereza nyumba 9,500 na mara baada ya mpango huo kukamilika tunategemea kumaliza kero za makazi ya Askari Magereza nchini likiwemo Gereza alilolitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeendelea na mpango wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba kwenye baadhi ya Magereza na kujenga nyumba mpya. Ni nia ya dhati ya Serikali kuendelea kuboresha nyumba za Askari nchini zikiwemo za Gereza la Kingulungundwa kwa awamu. Kwa sasa, Jeshi la Magereza linajenga nyumba 320 za Maafisa na Askari hapo Ukonga na fedha ambayo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshatoa ni shilingi bilioni 10 na shilingi bilioni tano tayari zilishatolewa kwa ajili ya ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara inayotoka barabara kuu ya Dar es Salaam kuelekea Gereza la Kingurungundwa imekuwa haipitiki kwa gari wakati wa masika. Kimsingi barabara hiyo ipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Lindi vijijini na ndiyo yenye jukumu la kuifanyia matengenezo barabara hiyo kwa kuwa haiishii Gerezani tu, bali inaendelea kwenye vijiji vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza limeshafanya mawasiliano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijini ili barabara hiyo iweze kutengenezwa na kuepusha adha inayojitokeza wakati wa masika.