Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 8 Sitting 1 Energy and Minerals Wizara ya Nishat 09 2017-09-05

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Wilaya ya Urambo inapokea umeme kutoka kwenye kituo cha kupoozea umeme cha Kaloleni umbali wa kilometa 90 kufika Urambo ambako ndiko kiliko kikata umeme inapokuwa kumetokea tatizo katika njia. Aidha, chanzo hicho cha umeme pia kimetegemewa na Wilaya ya Kaliua, Jimbo la Ulyankulu na vijiji vya Ikomwa, Igange, Tumbi, Ilolangulu hadi Ugoola (Tabora na Uyui); uzoefu unaonyesha kwamba kama kukitokea tatizo la kiufundi katika njia huwa inasababisha kukatika kwa umeme katika njia nzima likiwemo Jimbo la Urambo na kusababisha malalamiko mengi kwa TANESCO.
Je, kwa nini Serikali isijenge kituo cha kupoozea umeme (substation) karibu na Wilaya ya Urambo ili kiweze kutoa umeme wa uhakika katika Wilaya hiyo inayozidi kukua katika mahitaji ya umeme hasa katika kutekeleza sera ya viwanda na katika taasisi zinazotoa huduma za kijamii kama hospitali, shule na kadhalika kwenye Jimbo hilo?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Tabora na Kigoma kwa kujenga njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 133 yenye urefu wa kilometa 372 kutoka Tabora kupitia Urambo, Kaliua, Uvinza na hatimaye Kigoma.
Mheshimiwa Spika, katika mradi huu, kituo cha kupoza umeme (substation) cha kilovoti 132 kitajengwa kati ya Urambo na Kaliua kitakachosafirisha umeme katika Wilaya ya Urambo, Kaliua, Uvinza hadi Kigoma na hivyo kuimarisha miundombinu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu wa mradi huu ulianza mwezi Juni, 2017 na utakamilika mwezi Septemba, 2017. Ujenzi rasmi wa mradi unatarajiwa kuanzia mwezi Aprili, 2018 na kukamilika mwezi Agosti, 2018. Mradi huu utagharimu shilingi bilioni 179.