Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 7 | Sitting 51 | Information, Culture, Arts and Sports | Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo | 418 | 2017-06-20 |
Name
Amina Saleh Athuman Mollel
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania na vyombo vyetu vya habari havina wakalimani wa lugha ya alama kwa ajili ya kuwawezesha viziwi kupata habari kwa uelewa uliotimilifu kama raia wengine.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa vyombo vya habari hasa tv vinaajiri wakalimani hasa katika taarifa za habari ili waweze kufuatilia matukio yanayooneshwa?
Name
Anastazia James Wambura
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Amina Saleh Mollel (Mbunge), kwa kuona umuhimu wa suala hili pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote hasa Mheshimiwa Stella Alex Ikupa (Mbunge) ambaye naye aliuliza swali hili tarehe 08/05/2017 katika mjadala wa bajeti ya Wizara yetu.
Napenda kulitaarifu Bunge lako kuwa baada ya swali la Mheshimiwa Stella Alex Ikupa Mbunge, Wizara iliitisha kikao cha wadau mbalimbali wakiwepo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, VETA, Chama cha Wakalimani wa Lugha za Alama (TASLI), TBC na wadau wengine ili kutafakari namna ya kutekeleza kwa haraka azma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine, tulikubaliana kwamba VETA watoe mafunzo hayo kwa kushirikiana na CHAVITA na TASLI, kutokana na mtandao mkubwa ambao VETA wanao na VETA wamekubali. TASLI wamepewa kazi ya kuandaa kanzi data za wakalimani wa lugha ya alama kwa viziwi, na TCRA wanaandaa kalenda yaani road map ya utekelezaji wa matumizi ya huduma za wakalimani wa lugha ya alama katika vituo vya televisheni nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hatua hizo TBC inaendelea na mawasiliano yake na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa - Taasisi ya Elimu ya Juu, inayofundisha wataalamu wa lugha ya alama kuona ni namna gani shirika linavyoweza kuwatumia wataalamu, wahitimu na wanafunzi wa chuo hicho kutoa kwa muda huduma ya lugha ya alama kupitia TBC.
Aidha, Serikali imeandaa kutekeleza suala hili kwa kuweka wakalimani wa lugha ya alama katika matukio ya Kitaifa kama maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano yaliyofanyika 26 Aprili, 2017. Vilevile TBC iko kwenye mchakato wa kuajiri wakalimani wachache kwa kuanzia wa lugha za alama kwa taarifa zake za habari na katika matangazo machache yanayorushwa na televisheni hiyo ya TBC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari binafsi nchini nao kuanza mchakato wa kuwaajiri wakalimani wa lugha ya alama ili waweze kuwawezesha watu wa kundi hili kupata taarifa kupitia vyombo vyao habari.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved