Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 52 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 431 2017-06-21

Name

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Misitu ya Hifadhi ndani ya Wilaya ya Same ni Msitu wa Shengena ambao ni chanzo cha Mito mikubwa ya Nakombo, Hingilili, Yongoma na Saseni ambayo maji yake yanatumiwa na wakazi wa Majimbo ya Same Mashariki, Mlalo na Korogwe Vijijini:-
• Je, ni lini Serikali itaanzisha doria kulinda Msitu wa Shengena kuzuia uharibifu unaoendelea ikiwemo uchomaji moto ambao pia unaathiri maisha ya watu?
• Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha utaratibu wa uvunaji wa miti iliyokomaa katika Msitu wa Shengena na kuweka mkakati wa kuotesha miti mingine ili msitu uwe endelevu?
• Je, Serikali inasema nini juu ya athari za kimazingira zinazotokana na uchimbaji wa madini ya Bauxite unaoendelea katika Msitu wa Shengena?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali ya Wilaya ya Same imekuwa ikitekeleza shughuli za doria na operations za mara kwa mara katika hifadhi za misitu ambapo wahalifu wanaopatikana na hatia ikiwa ni pamoja na uchomaji moto huchukuliwa hatua za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa kuwa uharibifu wa misitu unahusisha baadhi ya wananchi wasiozingatia Sheria, Serikali inakamilisha mpango wa usimamizi shirikishi na wananchi wa vijiji vyote 23 alivyovitaja vinavyopakana na hifadhi ya Chome ushiriki ambao utaboresha ulinzi wa hifadhi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, uhifadhi wa misitu ya mazingira asilia pamoja na mambo mengine unazingatia kutokuvuna miti hata baada ya kukomaa na pia kuacha miti ya asili iendelee kuota yenyewe badala ya kupanda miti mingine ili kulinda hifadhi na kuendeleza mfumo wa kiikolojia na bioanuwai zilizopo ndani ya hifadhi. Aidha, hatua hii inalenga kutunza, kuhifadhi na kuendeleza mfumo wa ikolojia ikiwa ni pamoja na vyombo vya maji na viumbe hai waliopo.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa madini katika maeneo ya hifadhi husimamiwa na sheria zikiwemo Sheria za Madini ya mwaka 2010, Sheria ya Misitu namba 14 ya mwaka 2002 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) ya mwaka 2004.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hakuna taarifa rasmi zinazohusu uchimbaji wa madini ya Bauxite katika Hifadhi ya Msitu wa Shengena. Aidha, iwapo mtu yoyote binafsi au taasisi itahitaji kufanya shughuli za uchimbaji madini ndani ya hifadhi hiyo, atatakiwa kufuata taratibu za kisheria zitakazozingatia masuala yote muhimu ikiwemo kufanyika kwa tathmini ya athari ya mazingira kabla ya kuanza kwa uchimbaji huo.