Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 23 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 192 2018-05-07

Name

Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Primary Question

MHE. MARY P. CHATANDA (K.n.y. MHE. HAMOUD A. JUMAA) aliuliza:-
Serikali iliahidi kuwapa fidia wananchi waliopisha njia ya mradi wa umeme wa gesi toka Kinyerezi kwenda Arusha, Awamu ya Kwanza hadi Chalinze lakini hadi sasa wananchi hao hawajalipwa fedha zao.
Je, ni lini wananchi wa Kibaha watalipwa fidia kutoka katika fedha zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano shilingi bilioni mbili?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamoud Abuu Jumaa, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi hadi Arusha. Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilometa 664 pamoja na kilometa 40 kutoka Kibaha hadi Zinga na kilometa 60 kutoka Segera hadi Kange, Tanga. Mradi huu unahusisha ujenzi wa Vituo vya Kupoza Umeme vya Chalinze, Segera, Kange na Zinga, Bagamoyo. Mradi huu utajengwa kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 kazi ya utathmini wa mali za wananchi wa Kibaha na Chalinze ilifanyika ili waweze kulipwa fidia na kupisha ujenzi wa mradi. Kazi inayofanyika kwa sasa ni kukamilisha taratibu za malipo kwa wananchi waliohakikiwa. Zaidi ya shilingi bilioni 21.56 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wanaopitiwa na mradi katika maeneo ya Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na maeneo mengine yanayopitiwa na mradi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze. Fidia kwa wananchi hao italipwa mara tu baada ya taratibu za malipo hayo kukamilika.