Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 3 | Sitting 10 | Energy and Minerals | Wizara ya Nishat | 78 | 2016-05-02 |
Name
Hassan Elias Masala
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Primary Question
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwa na zoezi la utafiti katika Kata ya Nditi, Wilayani Nachingwea linalofanywa na kampuni tofauti:-
(a) Je, nini hatma ya utafiti huo wa muda mrefu ambao unaleta mashaka kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo?
(b) Je, wananchi wa maeneo jirani wanaweza kuruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji mdogo ili waweze kunufaika badala ya kuwa walinzi na vibarua?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta watafiti zaidi katika maeneo mengine ya Wilaya hizo kama Kiegei, Marambo, Nditi na kadhalika?
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa eneo la Nditi lililoko Wilaya ya Nachingwea limefanyiwa utafiti wa madini kwa muda wa zaidi ya miaka minane sasa, hasa madini ya nickel katika eneo la Ntaka Hill. Leseni ya utafutaji ya PL Namba 4422/2007 ilitolewa tarehe 7 Aprili, 2007 kwa kampuni ya Warthog Resources ambayo inatoka Australia ambayo kwa sasa inaitwa Nachingwea Nickel Limited.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2014 kampuni hii imetumia zaidi ya dola za Marekani milioni 36 na kugundua mashapo ya madini ya nickel takribani tani 356,000 na ya shaba tani 76,000 na upembuzi yakinifu unaonesha mashapo yanatosha kuchimba kwa mgodi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kuanguka kwa bei ya nickel kwenye Soko la Dunia kumesababisha kampuni kutoanzisha mgodi wa uchimbaji mapema. Kampuni inakusudia kuanzisha mgodi huo mara baada ya bei ya nickel kuimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu Namba 14 cha Sheria ya Madini ya 2010, kinamzuia mtu yeyote asiye na leseni halali ya kuchimba madini, kufanya hivyo. Namuomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu tushirikiane kuelimisha wananchi ili kutovamia maeneo kuchimba madini kiholela bila kuwa na leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Lindi kuna kampuni 98 zenye jumla ya leseni 213 za utafutaji mkubwa wa madini. Madini yanayofanyiwa utafiti ni pamoja na nickel, dhahabu, graphite, gypsum, manganese pamoja na beach sands.
Sehemu kubwa ya maeneo aliyotaja Mheshimiwa Mbunge, ya Kiegei, Marambo na Nditi ni baadhi ya maeneo ambayo leseni hizi za utafutaji zipo. Tunashauri pia wananchi wa maeneo hayo watumie fursa ya uwepo wa makampuni haya kushirikiana nayo katika shughuli za utafiti. Aidha, Wakala wa Jiologia Tanzania (GST) wanaendelea kufanya utafiti wa madini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Nachingwea.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved