Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 48 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 409 2018-06-11

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Serikali kupitia Kanuni mbalimbali za Utumishi inatambua mtumishi wa mke au mume na watoto au wategemezi wanne. Hata hivyo, utumishi wa umma hautambui baba wala mama hasa linapotokea tatizo la msiba, mara zote huduma ya misiba ya wazazi imekuwa ni jukumu la mtumishi mwenyewe:-
Je, ni lini Serikali itawajumuisha wazazi wa mtumishi kama wanufaika wa huduma mbalimbali anazopata mtumishi wa umma?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato Chumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma, Toleo la Mwaka 2009, huduma ya mazishi hutolewa kwa mtumishi mwenyewe na wategemezi wanne. Serikali haigharamii mazishi ya baba au mama wa mtumishi kutokana na ukweli kwamba wapo wazazi wenye watoto zaidi ya mmoja katika utumishi wa umma na katika maeneo tofauti nchini. Endapo kwa mfano wazazi wa mtoto zaidi ya mmoja ambao katika utumishi wa umma watafariki Serikali ingelazimika kulipa gharama pengine mara tatu au zaidi kwa kuwa hakuna mfumo madhubuti wa kutambua watu ili kubaini wazazi wenye watoto zaidi ya mmoja katika utumishi wa umma. Kwa kuwa sasa Serikali haina mfumo jumuishi wa utambuzi na udhibiti wa taarifa hizi ingelipa gharama kubwa za huduma za mazishi za mara nne au mara tano au mara tatu kwa mzazi mmoja aliyefariki.
Mheshimiwa Spika, ili kuziba pengo lililopo la kuhudumia mazishi ya wazazi, Serikali imeruhusu watumishi wenyewe kuchangiana kupitia vyama vya hiari ambapo michango yao hufunguliwa akaunti maalum ili inapotokea misiba ya wazazi waweze kupeana rambirambi katika Mifuko ya Kufa na Kuzikana. Kupitia mifuko hii, watumishi wanapofiwa na ndugu zao wa karibu wakiwepo wazazi huwa wanapewa rambirambi. Aidha, huwa kuna michango ya rambirambi ya papo kwa papo inayosaidia gharama za misiba ya watumishi na ndugu wa karibu wakiwemo wazazi, na endapo wazazi wapo mbali na vituo vya kazi watumishi hupewa ruhusa maalum ya siku 14 kushiriki katika misiba.