Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 50 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 424 2018-06-13

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto ina hospitali moja ya Wilaya ambayo inabeba mzigo mkubwa sana wa watu. Aidha, wodi ya wajawazito ni chumba kidogo sana na hakuna kabisa wodi ya mama na mtoto. Je, ni lini Serikali itajenga vyumba hivyo?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Hospitali ya Wilaya ya Lushoto bado ina changamoto ya msongamano katika wodi za akina mama wajawazito kwa sababu haina eneo la kutosha kukidhi wingi wa akina mama wajawazito wanaohudumiwa. Wodi ya akina mama wajawazito iliyopo imetokana na uamuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kubadilisha matumizi ya baadhi ya majengo ili yatumike kama wodi ambapo jumla ya shilingi milioni 30 zilitumika katika mwaka wa fedha 2016/2017 kutengeneza wodi tatu ndogo ndogo yaani wodi ya akina mama wajawazito kabla ya kujifungua, wodi ya akina mama wajawazito baada ya kujifungua yenye uwezo wa kuhudumia akina mama sita kwa wakati mmoja, chumba cha upasuaji chenye vitanda vitatu vya upasuaji na wodi ya akina mama na watoto wachanga baada ya kujifungua kwa kawaida au upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukabiliana na changamoto hiyo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepeleka shilingi milioni 400 katika Kituo cha Afya cha Mlalo; shilingi milioni 500 katika Kituo cha Afya cha Mnazi na shilingi milioni mia tano katika Kituo cha Afya cha Kangagae.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa matumizi ya fedha hizo ni kujenga vyumba vya upasuaji, wodi za mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua na maabara kwa lengo la kuboresha huduma kwa mama wajawazito ikiwemo huduma za dharura za upasuaji kwenye maeneo hayo, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano kwenye Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa wodi ya kisasa ya wajawazito (maternity complex) ni miongoni mwa vipaumbele vya juu vya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ndiyo maana katika mwaka wa fedha 2018/2019 imetenga shilingi milioni 25 kuanzisha ujenzi unaotarajiwa kukamilika mwaka 2019/2020.