Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 14 Sitting 7 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 81 2019-02-05

Name

Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Primary Question

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-

Wafungwa wakimbizi toka nchi za Burundi na DRC wamekuwa wakijaza mahabusu na magereza yetu:-

(a) Je, kwa nini Serikali isikubaliane na nchi za Burundi na DRC kubadilishana wafungwa ili wakimbizi hao wafungwe katika nchi zao?

(b) Je, wafungwa wa aina hiyo wanapokuwa mahabusu na magereza, Shirika la UNHCR linachangia gharama kwa kiasi gani?

(c) Je, UNHCR imechangia fedha kiasi gani kwa wafungwa wakimbizi waliofungwa au kuwekwa mahabusu nchini kuanzia mwaka 2017/2018?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nichodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Mwenyekiti, suala la kubadilishana wafungwa baina ya nchi moja na nyingine huongozwa na mkataba wa makubaliano ulioingiwa baina ya nchi moja na nyingine. Lengo la mkataba huo ni kumpa fursa mfungwa anayetumikia kifungo chake gerezani kutumikia sehemu ya kifungo chake kilichobaki katika nchi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ieleweke kuwa ni utamaduni wa kisheria duniani kwamba mahabusu na mfungwa bila kujali kama ana hadhi ya ukimbizi, wanapopokelewa na kuhifadhiwa katika magereza, jukumu la kuwatunza hufanywa na Serikali ya nchi husika. Serikali yetu imekuwa ikifanya hivyo kwa kufuata Sheria na Kanuni za Magereza zilizopo ambazo kimsingi zimeipa Serikali jukumu hilo. Aidha, ifahamike kuwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Magereza hakuna mahabusu au mfungwa mkimbizi kwani wahalifu wote hupokelewa kwa hati kutoka Mahakama zetu zenye utambulisho wa hadhi ya mahabusu au mfungwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa misingi hiyo suala la Shirika la UNHCR kuchangia gharama za kuwatunza wafungwa na mahabusu wanaodaiwa kuwa ni wakimbizi huwa halipo na halifanyiki kwa sababu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Magereza zilizopo hazijaainisha kumtambua mahabusu au mfungwa mkimbizi katika magereza yetu.