Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 14 Sitting 7 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 82 2019-02-05

Name

Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-

Tangazo la Serikali Namba 257 kifungu cha 6 kinaelekeza faini za makosa ya barabarani kulipwa kwa Askari aliyeandika faini au kwa OCD au Ofisi ya Mhasibu aliyeko karibu. GN hiyo imetoa nafasi ya kulipa ndani ya siku saba (7) na iwapo faini haitalipwa ndani ya siku saba (7) mkosaji atafikishwa Mahakamani ndani ya siku 10:-

(a) Kwa nini Askari wa Usalama Barabarani huamua kushikilia magari ya wanaokamatwa wakati huohuo, wakati sheria inasema walipe ndani ya siku saba (7)?

(b) Katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna mashine za kielektroniki (POS) za kulipia faini na ANPR ambayo husaidia kufuatilia ambao wanakwepa kulipa faini walizoandikiwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza upatikanaji wa POS na ANPR ili kuepusha mifarakano na usumbufu unaojitokeza?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kifungu cha 6 cha Tangazo la Serikali Namba 257 alichokinukuu kilishafanyiwa marejeo mwaka 2015 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali mnamo tarehe 30/01/2015 na kuwa Kanuni namba 30/2015 ya Sheria ya Usalama Barabarani ambayo imelenga kutengeneza mfumo wa ulipaji wa tozo za papo kwa papo kwa njia ya kielektroniki. Kanuni hii pia inasomwa pamoja na Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002, kifungu cha 95.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukamataji wa magari na kisha kuyashikilia upo kisheria, kifungu cha 87, kifungu kidogo cha (a), (b) (c) na (d) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002, magari haya hushikiliwa kulingana na uzito wa kosa alilofanya dereva mfano makosa hatarishi kama ubovu wa gari ambapo gari linatakiwa likafanyiwe ukaguzi na Mkaguzi wa Magari, makosa ambayo dereva au mmiliki anatakiwa apelekwe Mahakamani na kadhalika.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa ulipaji tozo za papo kwa papo kwa njia ya mtandao ulianza kutekelezwa kwa majaribio katika Mikoa mitatu ya Kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Temeke ambapo jumla ya mashine za kielektroniki (POS) 360 na kamera za kufuatilia magari yanayodaiwa faini (ANPR) 3 zilizotumika na kuonyesha ufanisi na mafanikio makubwa. Kuanzia Apili, 2018, mfumo huu ulianza kutumika nchini kote ambapo mashine hizi za kielekroniki (POS) zipatazo 3,000 zilipelekwa mikoa yote nchini na mashine za ufuatiliaji wa magari (ANPR) zipatazo 400 zinatarajia kusambazwa mikoa yote nchini kuondoa usumbufu usio wa lazima.