Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 session 13 Sitting 2 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 16 2018-11-07

Name

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Hali ya sekta ya kilimo na mifugo katika Jimbo la Same Mashariki ni mbaya licha ya kuwepo wafanyakazi wa Serikali wanaosimamia sekta hizo kwenye Wilaya, Kata na hata Vijiji. Wengi wa wafanyakazi hao wanatumia muda mwingi kufanya kazi zao binafsi badala ya kuwasaidia wakulima na wafugaji kuleta mabadiliko katika sekta hizo.
(a) Je, Serikali inatumia kigezo gani kutathmini utendaji kazi wa waajiriwa hao kupima ufanisi wao?
(b) Je, Serikali ipo tayari kupunguza idadi ya waajiriwa hao waliopo vijijini ili fedha itakayookolewa kutoka katika mishahara yao isaidie kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji na malambo?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuwasimamia maofisa ugani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara za Kisekta hutoa miongozo inayoainisha viwango vya kitaalam na ikama. Mamlaka za Serikali za Mitaa husimamia masuala ya kiutawala na utendaji kazi wa siku kwa siku ikiwemo kupima ufanisi na tija kwa kutumia Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Watumishi wa Umma (Open Performance and Review Appraisal System – OPRAS) ambapo kila mtumishi hukubaliana na mwajiri kuhusu malengo yatakayotekelezwa kwa mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa maafisa ugani wa kilimo na mifugo nchini, badala ya kupunguza idadi yao, mpango uliopo kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 22(b) ni kuongeza idadi ya Maafisa Ugani kutoka 9,558 waliokuwepo mwaka 2014 hadi 15,082 ifikapo mwaka 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwakumbusha maafisa ugani wote na wasimamizi wao kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yaliyowataka Maafisa Ugani kutokaa ofisini na badala yake kwenda vijijini kuwasaidia wakulima na wafugaji. Nazikumbusha mamlaka za nidhamu kuchukua hatua kali dhidi ya Maafisa Ugani wazembe wasiowajibika kwa umma.