Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 17 Energy and Minerals Wizara ya Madini 139 2019-04-29

Name

Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Primary Question

MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-

Uwepo wa madini ya chokaa umedhihirika katika Kijiji cha Ausia, Kata ya Suruke, Jimbo la Kondoa Mjini, kwa muda mrefu sasa, katika jitihada za kujaribu kunufaika wananchi wamekuwa wakichimba madini haya kienyeji:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Wataalam kufanya utafiti kubaini kiwango cha uwepo na ubora wa madini hayo ya chokaa ili wananchi wa maeneo hayo waanze kunufaika sasa na rasilimali hiyo muhimu?

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) hufanya utafiti wa awali wa madini (Regional Geological Mapping) na kuandaa ramani kupitia QDS yaani quarter degree sheet na taarifa za kijiolojia nchini. Utafiti huo wa awali husaidia kutangaza fursa za uwepo wa madini yanayogunduliwa ili wawekezaji binafsi wa madini wa nje ya nchi waweze kuwekeza katika tafiti za kina na uchimbaji. Hadi kufikia mwaka 1999, GST ilifanya utafiti wa Kijiolojia katika Wilaya ya Kondoa na kutengeneza Ramani za Kijiolojia yaani hizo QDS zipatazo sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ikiwemo Kampuni ya Beak Consultants GmbH ya Ujerumani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 2013 na 2014 ilifanya utafiti wa awali na kubainisha uwepo wa madini ya chokaa katika Vijiji vya Ausia na Tumbelwa, madini ya nickel katika Kijiji cha Ausia, madini ya dhahabu katika Vijiji vya Mpondi, Maji ya Shamba, Birise, Chang’aa, Jogolo, Tumbelo na Forya na madini ya shaba katika Kijiji cha Masange.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itazidi kuiwezesha GST na STAMICO kuendelea kufanya tafiti za kina kadri itakavyoweza kupata bajeti ya kutosha kama ilivyokwishafanya katika maeneo ya Tanga, Chunya, Katente, Mpanda, Kyerwa na Buhemba ili wananchi wanufaike na rasilimali za madini na kuwawezesha kuongeza kipato, kupunguza umaskini na kuongeza pato la Taifa kwa kulipa kodi stahiki.