Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 19 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 156 2019-05-02

Name

Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Primary Question

MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi katika mazingira magumu sana kutokana na uchakavu wa vitendea kazi pamoja na kukosekana kwa magari ya kutosha:-

(a) Je, ni lini Serikali itawapatia magari Askari Polisi wa Wilaya ya Masasi kutokana na kutokuwa na magari ya kutosha?

(b) Je, ni lini Serikali itarekebisha utaratibu uliopo ambapo askari wanalazimika kutoa pesa zao za mfukoni kuwapa chakula mahabusu?

(c) Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za askari katika Wilaya ya Masasi?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uhaba wa vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na uchache wa magari. Kwa sasa Wilaya ya Masasi imeshapatiwa gari moja aina ya Leyland Ashok, hivyo kufanya kuwepo kwa magari matatu ambayo ni PT 1865, Toyota Landcruiser, PT 4011 Grand Tiger na Leyland Ashok. Gari hili jipya litatumika kwa shughuli mbalimbali kama doria na operesheni kubwa. Aidha, kutokana na jiografia ya Wilaya ya Masasi, Jeshi la Polisi litaiongezea Wilaya ya Masasi magari kwa kadri yatakavyopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna utaratibu waAskari Polisi kutoa pesa zao mfukoni kwa ajili ya chakula cha mahabusu, bali utaratibu uliopo ni kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuwapatia chakula mahabusu waliopokorokoroni ingawa pia ndugu za mahabusu wanaruhusiwa kuwapelekea chakula jamaa zao walioko korokoroni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Masasi ina nyumba za makazi ya askari zipatazo 15 ambazo zinaishi familia za askari 30, ingawa ni kweli askari wengine wapatao 154 bado wanaishi uraiani. Hata hivyo, Serikali itaendelea kujenga nyumba za makazi ya Askari kwa awamu kwa kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu.