Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 16 | Sitting 4 | Energy and Minerals | Wizara ya Nishati | 50 | 2019-09-06 |
Name
John Peter Kadutu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) unaendelea kote nchini. Katika Jimbo la Ulyankulu bado umeme haujafika katika maeneo mengi:-
(a) Je, ni lini sasa umeme utasambazwa katika Kata za Uyowa, Silambo, Igombe Mkulu, Seleli, Nhwande na Kanoge?
(b) Hivi karibuni Wilaya ya Kaliua imesajili Shule za Sekondari tano (5) na Vituo vya Afya pamoja na Sekondari ya Mkondo; je, ni lini sasa umeme utafikishwa katika taasisi hizo?
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vijiji 49 vya Jimbo la Ulyankulu kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza unaoendelea. Jumla ya Vijiji 19 vinatarajiwa kupatiwa umeme ambavyo ni Mwongozo, Mapigano, Mwanduti, Kanoge, Utamtamke, Iyombo, Ikonongo, Mbeta, Kagera, Ulanga, Imara, Kanindo, Nhwande, Keza, Mkiligi, Ilege, Konane, Busondi na Seleli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 127.96; njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 76; ufungaji wa transfoma 38 za KVA 50 na KVA 100 pamoja na kuunganishia umeme wateja wa awali 1,246. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 6.8 na kwa sasa mkandarasi JV Pomy Octopus na Intercity anaendelea na kazi mbalimbali za miundombinu ya umeme katika kata 12 zikiwemo Kata za Kanoge, Nhwande, Seleli na Igombe Mkulu. Kazi za kufikisha umeme katika vijiji hivyo itakamilika ifikapo mwezi Juni, 2020.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza, taasisi zote za huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu na maji zinapewa kipaumbele. Kwa sasa mkandarasi anaendelea na kazi ya kupeleka umeme katika Kituo cha Afya cha Mkondo na Shule ya Sekondari Mkondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved