Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 17 Sitting 1 Water and Irrigation Wizara ya Maji 10 2019-11-05

Name

James Kinyasi Millya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Primary Question

MHE. JAMES K. MILLYA aliuliza:-

Kuna mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mkoa wa Kilimanjaro kuelekea Arusha Mjini, mradi huu unapitia kwenye mipaka ya Wilaya ya Simanjiro Kata za Naisinyai na Mererani.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wananchi wa Kata hizo wanapatiwa huduma hiyo inayopita kwenye maeneo yao;

(b) Mheshimiwa Rais alipokuwa akizindua ujenzi wa barabara ya kilometa 14 toka KIA hadi Mererani aliwaahidi Wananchi wa Mererani na Naisinyai kwamba atawakumbuka kwenye kuondoa adha ya maji; Je, Serikali imejipangaje kutimiza ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Kinyasi Millya Mbunge wa Simanjiro lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Arusha na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Arumeru. Mradi huu pia utatoa huduma ya maji katika maeneo ambayo bomba kuu la maji kuelekea Arusha litapita. Kata za Mererani na Naisinyai ni miongoni mwa kata hizo na vijiji vitakavyopata huduma ya maji ni Naepo, Oloshonyoke na Kibaoni ambavyo viko katika Kata ya Naisinyai na vijiji vya Songambele, Getini na Kangaroo ambavyo viko katika Kata ya Mererani.

Mheshimiwa Spika, katika kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuondoa adha ya maji katika maeneo hayo, mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Arusha na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Arumeru utahusisha kuboresha huduma ya maji katika kata za Mererani na Naisinyai. Mradi huu mkubwa wa maji kutoka Kilimanjaro kwenda Jiji la Arusha unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2020. Mradi utakapokamilika, adha ya maji katika maeneo hayo itakuwa ni historia.