Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 47 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 394 2019-06-18

Name

Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Primary Question

MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA kama ilivyoahidi katika vijiji vya Munjere, Baraka, Mbaasha, Lepurko, Mti Mmoja, Arkatan, Arkaria, Mfereji, Ndonyonaado, Mswakini, Naitolia, Emurua, Lashaine, Orkenswa, Engaaroji, Oldonyolengai na Naalarami?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Shule ya Sekondari Oldonyolengai ambayo laini imefika tangu mwaka 2015 lakini mpaka sasa umeme haujawaka?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Julias Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imedhamiria kufikisha ueme katika vijiji vyote visivyo na umeme nchini ifikapo mwezi Juni 2021. Kulingana na mpango wa kupeleka umeme katika vijiji 64 Wilayani Monduli vijiji 16 vilishapatiwa umeme vikiwemo vijiji vya Arkatani na Mti Mmoja ni miongoni mwa vijiji vya Wilaya ya Monduli vilivyopata umeme kupitia awamu ya pili ya mradi wa kusambaza umeme Vijijini (REA II). Aidha, vijiji vya Arkaria, Lepurko na Mbaasha vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea.

Mheshimiwa Spika, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 48.75 na njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 40 na ufungaji wa transfoma 20. Jumla ya wateja wa awali 720 wataunganishiwa umeme na gharama za mradi ni shilingi bilioni tatu. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2020.

Vijiji vingine vya Munjere, Baraka Mfereji, Ndonyonaado, Mswakini, Naitolia, Emurua, Lashaine, Orkenswa, Engaaroji na Naalarami vitapata umeme kupitia REA III mzunguko wa pili utakaoanza kutekelezwa kuanzia mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021.

(b) Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari Oldonyolengai iliyopo Kata ya Engaruka imeshapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea kutekelezwa Wilayani Monduli.