Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 2 | Sitting 9 | Finance and Planning | Wizara ya Fedha na Mipango | 118 | 2021-02-12 |
Name
Daimu Iddi Mpakate
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kusini
Primary Question
MHE. DAIMU I. MPAKATE Aliuliza:-
Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na nchi ya Msumbiji kwa upande wa Kusini.
Je, ni lini Serikali itafungua Ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA) Lukumbule?
Name
Mwanaidi Ali Khamis
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini kwa kutambua umuhimu wa kulipa kodi na hivyo kuhitaji huduma za kikodi zisogezwe karibu yao. Ni dhamira ya Serikali kutumia fursa kama hii kusogeza karibu huduma za kikodi kwa wananchi ili kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inao utaratibu wa kupitia na kufanya tathmini ya sehemu zote ambazo zinaweza kujengwa ofisi kwa ajili ya kurahisisha ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu unazingatia uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa pindi ofisi hizo zitakapofunguliwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mwenendo wa kukua kwa biashara kati ya Tanzania na Msumbiji, TRA inapenda kuwahakikishia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini kuwa imelichukua suala hili na italifanyia kazi kwa kutuma timu ya wataalam ili kufanya tathmini ya kina na endapo kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa kitakuwa kikubwa ikilinganishwa na gharama za ukusanyaji wa mapato, ujenzi wa ofisi katika eneo hilo utaanza haraka iwezekanavyo.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved