Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 3 | Sitting 8 | Works, Transport and Communication | Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi | 64 | 2021-04-13 |
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:-
Je, lini ni Serikali itatekeleza ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni ya kumaliza mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wananchi na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege KIA?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa mbele baada ya kupewa kura za kutosha na wananchi wa Tarime Vijijini, naomba niwashukuru sana kwa ushirikiano. Pia, namshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea na namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kuniamini na kunipa nafasi ya kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Ujenzi na Uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: - (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 1969 Serikali ilitenga eneo lenye ukubwa wa ekari 11,085 kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA). Eneo hilo lilipimwa mwaka 1989 kwa ramani ya upimaji Na. E255/18 iliyosajiliwa na namba 231264 inayofahamika kama FARM No.1 lenye Hati namba. 22270 iliyotolewa 20 Machi, 2005.
Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2001 Serikali ilibaini kuwepo kwa baadhi ya wananchi kutoka vijiji vinavyopakana na KIA vya Sanya Station, Chemka, Tindigani na Mtakuja vilivyopo Wilaya ya Hai na Vijiji vya Majengo, Samaria na Malula vilivyopo Wilaya ya Arumeru kuingia kwenye eneo la KIA na kuweka makazi ya kudumu.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilichukua hatua za kufanya tathmini shirikishi wa mali za wananchi ili kuwaondoa kwa lengo la kutimiza azma ya Serikali kuendeleza KIA na pia kulinda usalama wa Kiwanja. Katika utathmini huo, ilibainika kwamba ndani ya eneo hilo kuna kaya 289 zenye thamani ya fidia iliyotakiwa shilingi 426,020,500/=. Fedha za kulipa fidia hizo hazikuwepo wakati huo, kwa hiyo, fidia haikulipwa.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2013, 2018 na 2019 kwa nyakati tofauti, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kushirikisha TAMISEMI, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha, Ofisi ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Wilaya za Hai na Arumeru imekuwa ikishughulikia suala hili kwa kushirikiana na uongozi wa vijiji husika ili kupata suluhu kwa kubaini idadi ya kaya zenye makazi ya kudumu katika eneo la KIA na kufanya tathmini upya.
Mheshimiwa Spika, mwezi Juni, 2018 zoezi la uwekaji wa alama lilianza ambapo Vijiji vya Majengo na sehemu ya Kijiji cha Mtakuja viliwekwa alama za kudumu. Vijiji vya Samaria na Malula vilivyopo Wilaya ya Arumeru, Vijiji vya Tindigani na Sanya Station katika Wilaya ya Hai vilikataa kutoa ushirikiano kwa Timu ya Wataalam kwa kukataza wataalam katakata kuingia katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imejipanga kukamilisha zoezi hili kwa kurudishia mipaka ya kudumu ya KIA na kubaini idadi ya kaya zilizopo ndani na kufanya tathmini upya na kupata kiasi ambacho kinatakiwa kulipwa ili zoezi hili liweze kumalizika. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved