Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 25 Works, Transport and Communication Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 208 2021-05-07

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Primary Question

MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Nyololo – Mtwango – Mafinga hadi Mgololo?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Nyololo – Mtwango yenye urefu wa kilomita 40.4 na barabara ya Mafinga – Mgololo yenye urefu wa kilometa 81.14 zinasimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS). Barabara ya Nyololo – Mtwango ni barabara ya mkoa ya kiwango cha changarawe na barabara ya Mafinga – Mgololo ni barabara kuu ya kiwango cha changarawe na kiwango cha lami katika maeneo korofi. Barabara hizi zinapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya biashara na chakula na pia zinahudumia viwanda kadhaa ikiwa ni pamoja na Kiwanda cha Karatasi cha Mgololo.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nyololo – Mtwango kwa kiwango cha lami. Aidha, inaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mafinga – Mgololo kwa kiwango cha lami, ambapo kwa sasa kazi hii ipo katika hatua za mwisho.

Mheshimiwa Spika, barabara hizi zitaingizwa katika mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizi kwa kiwango cha lami, kwa sasa barabara hizi zinaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali kila mwaka ili kuhakikisha kuwa zinapitika katika majira yote ya mwaka. Ahsante.