Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 28 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 235 2021-05-12

Name

Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makanya kwenda kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same ina urefu wa kilometa 40.9. Kipande cha kilometa 4.5 cha barabara hii kimeinuliwa kwa kujengwa tuta kati ya kilometa 14.5 zinazotakiwa kujengewa tuta kwa kiwango cha changarawe. Kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika muda wote na ndiyo maana imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara.

Katika mwaka wa fedha 20219/2020, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Same umefanya matengenezo ya barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 3.54 kwa gharama ya shilingi milioni 77.36.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Same imefanya matengenezo ya barabara hiyo kipande chenye urefu wa kilometa mbili kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 49.4. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 61.25 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita moja pamoja na ujenzi wa makalavati 14.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi na itaendelea kuifanyia matengenezo ili kuhakikisha inapitika. Serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika bajeti zijazo ili kuiboresha na kurahisisha usafirishaji wa Jasi.