Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 36 Finance and Planning Wizara ya Fedha na Mipango 304 2021-05-25

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kusamehe kodi za miaka ya nyuma taasisi za dini 7 zilizokuwa zikiendeshwa kwa utaratibu usiolenga kupata faida na kuziwekea utaratibu taasisi hizo kuanza kulipa tangu walipojulishwa kutakiwa kulipa kodi?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria za kodi, taasisi za dini ambazo zinajiendesha kutokana na sadaka kutoka kwa waumini wao ama misaada inayotolewa na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, hazikatwi na hazitakiwi kulipa kodi ya mapato, isipokuwa taasisi zenye sifa kama hizo husajiliwa na kupewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa madhumuni ya kuziwezesha kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu Mamlaka ya Mapato kama vile kuwasilisha kodi zinazokatwa kutoka kwa watumishi wa taasisi hizo na usajili wa mali mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, aidha, taasisi za dini zinazofanya shughuli za kiuchumi kwa lengo la kujipatia faida kutokana na shughuli hizo zinatakiwa kusajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kama wafanyabiashara wengine na kulipa kodi ya mapato kulingana na faida inayopatikana.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipokea maombi ya kusamehe kodi za miaka ya nyuma kutoka taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi za dini. Serikali inaendelea kutathmini maombi hayo ili kuona hatua zinazoweza kuchukuliwa bila kuathiri matakwa ya sheria zilizopo.