Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 3 | Sitting 55 | Water and Irrigation | Wizara ya Maji | 458 | 2021-06-21 |
Name
Stella Simon Fiyao
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Mradi mkubwa wa maji katika Mji wa Tunduma ili kutatua changamoto wanayoipata wakazi wa mji huo?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tunduma unapata maji kutoka kwenye visima virefu tisa vilivyoko maeneo ya Ikulu, Sogea, Mamboleo, Tazara, Maporomoko, Mahakamani, Majengo, Msongwa na Makambini. Visima hivyo vinazalisha maji lita 2,072,000 kwa siku wakati mahitaji ya maji kwa Mji huo ni lita 4,413,000 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha huduma ya maji safi na salama katika Mji wa Tunduma, Serikali inatekeleza mipango ya muda mfupi na muda mrefu, ambapo katika mpango wa muda mfupi mwaka 2020/21, Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imechimba visima virefu sita vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita 600,000 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji ya visima hivyo utafanyika kuanzia mwezi Julai, 2021, na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba, 2021. Vilevile, Serikali itafanya upanuzi wa mtandao wa maji katika maeneo mengine ya Mji wa Tunduma ikiwemo maeneo ya pembezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu wa kuboresha huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza katika Mji wa Tunduma, Serikali imepanga kujenga mradi kupitia chanzo cha maji cha Mto Bupigu uliopo Wilaya ya Ileje wenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha lita milioni 73 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina (detailed design) wa mradi huo anatarajiwa kupatikana katika robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2021/2022. Aidha, Serikali itaendelea kufanya utafiti wa vyanzo vya maji juu na chini ya ardhi ili kupata maji yenye kutosheleza katika Mji wa Tunduma na miji mengine hapa nchini.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved