Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 4 | Sitting 8 | Regional Administration and Local Government Authorities | Ofisi ya Rais TAMISEMI. | 96 | 2021-09-09 |
Name
Dr. John Danielson Pallangyo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Mashariki
Primary Question
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara zinazopanda milimani Arumeru Mashariki ili kuwafikishia Wananchi huduma pamoja na kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara kwa barabara hizo ambapo gharama zake ni kubwa kutokana na ugumu wa kijiografia?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imeidhinisha jumla ya shilingi bilioni 1.93 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za milimani zenye jumla ya urefu wa kilomita 82.1 pamoja na barabara za ukanda wa chini zenye jumla ya urefu wa kilomita 22.3 kwa kiwango cha changarawe, kujenga daraja moja, makalavati 63 pamoja na kuchimba mifereji ya kuondoa maji barabarani yenye urefu wa kilomita nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, barabara zenye urefu wa kilomita sita za ukanda wa milimani zitafanyiwa usanifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami. Barabara hizo ni Leganga – Mulala kilomita mbili; Police – Magarisho kilomita mbili; Sangisi – Ndoombo kilomita mbili kwa gharama ya shilingi milioni tano kwa ajili ya usanifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021, Serikali ilifanya matengenezo ya barabara za Maji ya Chai – Sakila kilomita tatu; Police – Ngurdoto kilomita 3.5; Mji Mwema – Dispensary kilomita 0.5; Leganga – Ngarasero kilomita 0.8; Kisimiri Sekondari kilomita nne; Ngarenanyuki –Ngabobo kilomita 2.5; Ubungo – Irrikolanumbe kilomita 2.6; Sangisi – Ndoombo kilomita tano; Tengeru – Nambala kilomita mbili; Poli – Seela kilomita mbili pamoja na ujenzi wa barabara ya Sangis – Nambala kilomita 1.9 kwa kiwango cha lami kwa jumla ya gharama ya shilingi bilioni 1.38.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa barabara zinazopanda milimani Arumeru Mashariki kadri ya fedha zinavyopatikana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved