Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 5 | Sitting 4 | Water and Irrigation | Wizara ya Maji | 42 | 2021-11-05 |
Name
Dr. Christine Gabriel Ishengoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -
Je, ni lini tatizo la maji litakwisha katika Mji Mdogo wa Mikumi?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifauatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa Mji wa Mikumi ni wastani wa asilimia 62.3. Mahitaji ya maji kwa sasa kwa Mji wa Mikumi ni takriban lita milioni 3.4 kwa siku ukilinganisha na uzalishaji wa maji wa lita 900,000 kwa siku. Katika jitihada za kumaliza tatizo la maji, Serikali ina mpango wa muda mfupi na muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda mfupi, katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, Serikali imepanga kuboresha Mradi wa Maji wa Msimba kwa kufunga pampu mpya, ujenzi wa tangi la ujazo wa lita 90,000 na kuongeza mtandao wenye urefu wa Kilometa 6.5. Maeneo yatakayohudumiwa na mradi huu ni pamoja na Mitaa ya Msufini, Ng’apa, Msimbakati na Miomboni. Vilevile, mpango huu wa muda mfupi unahusisha ujenzi wa Mradi wa Maji Rutwina ambao unahusisha uchimbaji wa kisima kipya, ufungaji wa pampu na ulazaji wa bomba kuu umbali wa Kilometa 1.5 kutoka kwenye kisima hadi kwenye tanki la kuhifadhi maji eneo la Kidoma Mlimani. Maeneo yatakayohudumiwa ni pamoja na Kikwalaza, Tambukareli, Kidoma na Chekereni. Utekelezaji wa miradi hii unatarajiwa kuanza mwezi Disemba, 2021 na kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2022.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda mrefu, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa kutumia chanzo cha Mto Madibila. Mradi huo utahudumia maeneo ya Chekereni, Kikwalaza, Kidoma, Tambukareli, Magoma, Mjimpya, Mowlem na Green. Zabuni ya kumpata Mkandarasi wa kujenga mradi huo, imetangazwa tarehe 21 Oktoba, 2021. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwezi Januari, 2022 na kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba, 2022.
Mheshimiwa Spika, miradi hiyo yote ikikamilika itamaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Mikumi na kufikia lengo la asilimia 95.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved