Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 6 | Sitting 2 | Finance and Planning | Wizara ya Fedha na Mipango | 8 | 2022-02-02 |
Name
Agnesta Lambert Kaiza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukutana na Wafanyabiashara na kutafuta namna bora ya kuwa na utaratibu wa ukadiriaji kodi wenye usawa na unaozingatia mabadiliko ya biashara ili kulinda mitaji ya wafanyabiashara wa ndani?
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa idhini yako naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Rahim, ambaye ametujalia afya na uzima. Jambo la pili, nimshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Tatu ninaomba niwashukuru sana Wabunge wenzangu kwa ushirikiano wao mkubwa kwangu, dua na sala zao kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukadiriaji wa kodi hufanyika kwa mlipakodi kuandaa taarifa za biashara yake na mwisho wa mwaka kufanya makadirio ya kodi kulingana na taarifa hizo. Kwa msingi huo, mlipakodi hufanya makadirio mwenyewe (Self-Assessment). Kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kuhakiki usahihi wa makadirio aliyofanya mlipakodi endapo yamefuata matakwa ya sheria. Kwa hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania hukutana na walipakodi mara kwa mara kwenye michakato ya ukadiriaji wa kodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wafanyabiashara kujikadiria kodi wenyewe ni utaratibu unaotumika na kukubalika duniani kote. Utaratibu huu umewekwa kwa madhumuni ya kukuza mwamko wa ulipaji kodi kwa hiari (Voluntary Tax Compliance), kurahisisha ukusanyaji kodi na kupunguza gharama za ukadiriaji. Hata hivyo, biashara ambazo hazifuati misingi ya utunzaji kumbukumbu hulazimika kuingizwa kwenye utaratibu wa ukadiriaji kulingana na mauzo (Presumptive Tax System) ambapo TRA hutoa makadirio ya kodi kulingana na mauzo ya biashara husika katika kipindi cha mwaka. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved