Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 6 | Sitting 3 | Water and Irrigation | Wizara ya Maji | 23 | 2022-02-03 |
Name
Anatropia Lwehikila Theonest
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawapatia maji wananchi wa Wilaya ya Kyerwa kwa kutengeneza miundombinu ya kupeleka maji kwa Wakazi waishio sehemu za miinuko?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama Wilayani Kyerwa ni wastani wa asilimia 56.8. Katika kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa Wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na wale wanaoishi kwenye maeneo yenye miinuko, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mipya ya Kagenyi - Omukalinzi na Mabila. Ujenzi wa miradi hiyo unahusisha ulazaji wa bomba umbali wa Kilometa 7.2, matenki mawili yenye jumla ya ujazo wa lita 105,000 na vituo sita vya kuchotea maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi hii umefikia asilimia 70 na umepangwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2022. Sambamba na miradi hiyo, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuajiri Wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya Runyinya - Chanya, Kimuli - Rwanyango na Nyamiaga - Nyakatera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo, itahusisha ujenzi wa matenki matano yenye jumla ya ujazo wa lita 1,700,000, ulazaji wa mabomba umbali wa Kilometa 86.1 na ujenzi wa vituo 146 vya kuchotea maji. Kukamilika kwa miradi hiyo kutanufaisha Vijiji vya Nkwenda, Runyinya, Rwabwere, Muhurire, Karongo, Iteera, Muleba, Chanya, Chakalisa, Kagu na Nyakatera. Vijiji vingine ni Chakalisa, Kishanda, Nyakahita, Kyerwa, Nyaruzumbura, Milambi na Katera. Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imesaini mkataba mwezi Januari, 2022 na Mkandarasi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji Kijiji cha Murongo kwa kutumia fedha za UVIKO-19. Mradi huo unahusisha ujenzi wa tenki moja la lita 150,000, ulazaji wa mabomba umbali wa Kilometa 16.6, ujenzi wa vituo 25 vya kuchotea maji. Mradi huo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Juni, 2022. Kukamilika kwa miradi yote hiyo kutaboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Wilaya ya Kyerwa. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingine ili kuhakikisha kuwa huduma ya maji safi na salama ndani ya Wilaya ya Kyerwa inafikia kiwango kisichopungua asilimia 85 mwaka 2025.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved