Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 6 | Sitting 5 | Water and Irrigation | Wizara ya Maji | 52 | 2022-02-07 |
Name
Jonas William Mbunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafikisha maji safi na salama katika Kata za Kikolo, Utiri, Mbangamao, Kilimani na Mateka?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya Majisafi na salama katika Wilaya ya Mbinga ni wastani wa asilimia 59.2. Katika kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Mbinga, Serikali imeendelea kutekeleza Miradi ya Maji ya Mpepai, Mabuni, Amanimakolo, Luhagara, Myangayanga, Luwaita, Lifakara/Uzena na Ruanda. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Matangi kumi na moja (11) yenye jumla ya ujazo wa lita 775,000, ulazaji wa mtandao wa mabomba umbali wa kilometa 105.1 na ujenzi wa Vituo 116 vya kuchotea maji. Miradi hiyo ikikamilika itanufaisha wananchi wapatao 45,478.
Mheshimiwa Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mbinga yanapata huduma ya majisafi na salama na yenye kutosheleza. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imekamilisha kazi ya usanifu wa Miradi ya Maji katika Kata za Mateka, Kikolo na Utiri na ujenzi wa miradi katika Kata za Mateka na Utiri utaanza mwezi Aprili, 2022 na Mradi wa Maji wa Kikolo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2022/2023. Vilevile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji katika Kijiji cha Uzena (Kata ya Kikolo) kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO – 19 na unatarajia kukamilika ifikapo Juni, 2022.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kilimani inapata huduma ya maji kupitia mtandao wa maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbinga. Katika kuboresha huduma ya maji katika kata hiyo, Serikali imepanga kutekeleza upanuzi wa Mradi wa Maji wa Lifakara kupeleka Kata ya Kilimani katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved