Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 6 | Sitting 6 | Youth, Disabled, Labor and Employment | Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu | 54 | 2022-02-08 |
Name
Fakharia Shomar Khamis
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuwawezesha Wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao hawana ajira kulipa mikopo yao?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu mojawapo la msingi la Serikali ni kuandaa mazingira wezeshi kuhakikisha Watanzania wanapata maarifa na ujuzi wa kuwawezesha kujiajiri na kuajirika ili kukuza uchumi wa Taifa na vipato vyao. Kutokana na msingi huo, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilitunga Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Na. 9 ya Mwaka 2004 ambayo inawezesha kutoa mikopo au ruzuku kwa wanafunzi wahitaji waliokidhi vigezo.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, wazazi au wadhamini wanatakiwa kuhakikisha mikopo inarejeshwa ili iweze kunufaisha Watanzania wengine wanaohitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wanufaika wa mkopo ambao baada ya kumaliza vyuo wanachukua muda mrefu kupata ajira au kujiajiri, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri. Miongoni mwa hatua ambazo Serikali imezichukua ni pamoja na zifuatazo: -
(i) Kutoa mafunzo ya uzoefu wa kazini (internship) kwa wahitimu wa elimu ya juu nchini kupitia waajiri wa ndani na nje ya nchi ambapo jumla ya wahitimu 6,624 wamepatiwa mafunzo ya uzoefu wa kazini na wahitimu 11,475 wamepatiwa mafunzo ya kushindania fursa za ajira katika sekta mbalimbali za kiuchumi;
(ii) Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, jumla ya Shilingi bilioni 3.3 katika Serikali hii ya Awamu ya Sita, zimetolewa katika kipindi cha miaka ya nyuma mitano kwa ajili ya kuwapatia vijana mikopo nafuu wakiwemo wahitimu wa vyuo vikuu.
(iii) Kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri ya asilimia 10, jumla ya shilingi bilioni 145.8 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu;
(iv) Kutoa mafunzo ya ujasiriamali, kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, hadi sasa programu hii imewafikia vijana 8,736 wa elimu ya juu nchini;
(v) Kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa sekta binafsi ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ametilia mkazo sana eneo hili kuhakikisha kwamba tunapokuwa na uwekezaji na private sector kwa sababu ndiyo inaandaa watu wengi zaidi, vijana waweze kupata fursa ya kuajirika, kuajiriwa na kujiajiri. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved