Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 6 Sitting 12 Water and Irrigation Wizara ya Maji 146 2022-02-16

Name

Mohammed Maulid Ali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiembesamaki

Primary Question

MHE. MOHAMED MAULID ALI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kujikita zaidi kwenye uchimbaji wa Malambo ya kuhifadhia maji ya mvua na kujenga mabomba ya kuchukua maji toka kwenye maziwa na mito yote kuliko kuendelea kutumia gharama kubwa za kuchimba visima bila mafanikio?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Maulid Ali, Mbunge wa Kiembe Samaki, kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa uvunaji wa maji ya mvua kupitia mabwawa unatekelezwa kwenye maeneo mengi nchini ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, kazi ya ukarabati na ujenzi wa mabwawa na malambo inaendelea katika vijiji 20 vya Mlele, Kisarawe, Bunda, Kalambo, Mkinga, Handeni, Chalinze, Songwe, Chamwino, Chemba, Bahi, Kaliua, Kilindi, Itilima, Kishapu, Monduli, Kibaha na Kondoa. Aidha, kazi ya kuainisha maeneo 58 yanayofaa kujenga mabwawa madogo na malambo imefanyika na ujenzi utafanyika mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Serikali ni kuhakikisha miradi ya maji inajengwa kwa kutumia vyanzo vya uhakika ambavyo ni maziwa makuu na mito mikubwa. Mradi huo ni wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka Shinyanga, Kahama, Tabora, Igunga na Nzega Bukoba, Musoma, Misungwi na Magu. Vilevile, Utekelezaji wa miradi ya Mugango, Kiabakari, Butiama, Tinde, Shelui, na mradi wa maji katika miji ya Busega, Bariadi na Lagangabilili unaendelea kupitia Ziwa Victoria na mradi wa maji wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kupeleka Kigoma Mjini, Kirando na Kabwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, Serikali imeanza mpango wa kutekeleza miradi kupitia maziwa makuu ili kunufaisha maeneo ya pembezoni mwa maziwa hayo; kwa upande wa mito; mradi wa maji wa Kyaka - Bunazi ambao unatumia maji ya mto Kagera.

Mheshmiwa Naibu Spika, huduma ya maji yanayotokana na maji ya chini ya ardhi ni katika maeneo kame ambayo hayana vyanzo vya uhakika vya maji juu ya ardhi. Haya maeneo ni kama vile Dodoma, Singida, Lindi, Simiyu, Kigoma na Katavi.