Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 6 | Sitting 14 | Regional Administration and Local Government Authorities | Ofisi ya Rais TAMISEMI. | 161 | 2022-02-18 |
Name
Venant Daud Protas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kumalizia maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa ajili ya elimu, afya na polisi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa maboma 1,715 ya zahanti na vituo vya afya yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ambayo yanahitaji jumla ya shilingi bilioni 98.7 kwa ajili ya ukamilishaji wake. Aidha, katika sekta ya elimu kuna jumla ya maboma 12,101 ambayo yanahitaji jumla ya shilingi bilioni 183.5 kwa ajili ya ukamilishaji wake.
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 43.8 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati na vituo vya afya ambapo hadi kufikia Desemba, 2021 shilingi bilioni 29.5 zimepelekwa kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma hayo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/22 Serikali imetenga shilingi bilioni 79 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya madarasa na maabara ambapo fedha hizo tayari zimekwishapelekwa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya polisi 63 vilivyoanzishwa na wananchi kwa ajili ya kuimarisha huduma za usalama wa raia na mali zao katika maeneo yao ambapo hadi kufikia Desemba, 2021 shilingi bilioni 1.85 zimekwishatolewa sawa na asilimia 85. Mkakati wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha kwa awamu. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved