Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 9 | Sitting 10 | Youth, Disabled, Labor and Employment | Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu | 141 | 2022-11-11 |
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: -
Je, ni lini marekebisho ya sheria yataletwa Bungeni ili mwanamke anayejifungua mtoto njiti aongezewe likizo ya uzazi?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Kimataifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na.183 kuhusu haki ya uzazi unaelekeza nchi wanachama kuweka utaratibu wa kuwalinda mtoto na mama kutokana na changamoto za uzazi.
Mheshimiwa Spika, haki ya likizo ya uzazi kwa mwanamke mwajiriwa ipo kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Sura ya 366, Marejeo ya Mwaka 2019 kifungu cha 33 ambapo mwajiriwa mwanamke akijifungua mtoto mmoja anapewa likizo ya uzazi ya siku 84 na akijifungua watoto mapacha hupewa siku 100, kadhalika akijifungua mtoto njiti hupewa siku 84 katika mzunguko wake wa likizo.
Mheshimiwa Spika, uzoefu unaonesha kuwa wafanyakazi wanawake wanapewa likizo ya uzazi kwa mujibu wa sheria na endapo likizo itamalizika na bado kuna uhitaji wa kumlea mtoto njiti, mwajiriwa anapaswa kujadiliana na mwajiri wake na kukubaliana kuhusu nyongeza ya likizo.
Vilevile mzazi anapokuwa amelazwa hospitalini na mtoto anapaswa kupewa Exemption from Duty (ED) ambayo itamwezesha mwajiriwa huyo kuendelea kulea mwanaye bila kupoteza haki ya kulipwa mshahara wake endapo atawasilisha cheti cha daktari kwa mwajiri wake.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sheria haijaainisha utaratibu mahususi wa kumwezesha mwanamke mwajiriwa kupewa likizo ya uzazi baada ya kujifungua mtoto njiti, ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imelipokea suala hili na italifanyia kazi kwa kufanya maboresho katika kanuni za sheria husika kuwawezesha waajiri kuandaa sera za ajira ambapo pamoja na mambo mengine suala la likizo kwa mwanamke atakayejifungua mtoto njiti litaanishwa kwa lengo la kumlinda mtoto njiti na mzazi wake. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved