Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 7 Sitting 24 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 208 2022-05-17

Name

Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani kudhibiti magari yanayopakua na kupakia mizigo katika maeneo ya Kariakoo, Mtaa wa Msimbazi na Barabara ya Morogoro ili kupunguza kero kwa wakazi wa maeneo hayo?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti magari makubwa yanayopakia na kupakua mizigo katika maeneo ya Kariakoo, Mtaa wa Msimbazi na barabara ya Morogoro, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweka utaratibu wa kudhibiti magari hayo kwa kutoa vibali Maalum vinavyowaruhusu kuingia mjini kama ilivyotamkwa kwenye kifungu cha 8 cha Sheria Ndogo za Matumizi ya Barabara za Halmashauri ya Manispaa ya Ilala (ambayo ndiyo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa sasa) za mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, mtu yeyote atakayeingiza lori au kontena bila kibali atakuwa ametenda kosa, na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyopungua Shilingi elfu hamsini hadi laki tatu kulingana na uzito wa gari, au kifungo kisichozidi miezi 12 jela, au vyote kwa pamoja. Hata hivyo, halmashauri kwa kushirikiana na vyombo vingine, ina utaratibu wa kutoa elimu kwa madereva, wamiliki wa magari makubwa na kwa umma ili kuwapa uelewa wa athari zinazotokana na uingizaji wa magari makubwa kiholela.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ina mpango wa kujenga maegesho ya kisasa katika eneo la Mnazi Mmoja kwa ajili ya magari mbalimbali yakiwemo magari ya mizigo.