Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 11 Sitting 9 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo 118 2023-04-18

Name

Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Primary Question

MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha jamii inarudi katika maadili mema kutokana na ongezeko la mmomonyoko wa maadili?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kujibu swali kama Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba dakika moja niweze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kwa uhai na kila kinachotokea kwenye maisha yangu likiwemo na hili. (Makofi)

Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yangu Daktari Samia Suluhu Hassan kwa imani hii kubwa aliyonipa na nimuahidi ya kwamba nitatekeleza majukumu yangu kwa weledi tuwatendee haki wananchi tunao wahudumia. (Makofi)

Niwashukuru sana wananchi wa Muheza kwa kuendelea kuniunga mkono na ushirikiano mkubwa wanaonipa na niwahakikishie Muheza bado Mbunge mnaye na nitahakikisha nawaheshimisha. (Makofi)

Nikushukuru wewe Spika na Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania kwa miongozo na maelekezo ya kila mara, hili ni darasa kubwa na ninaendela kujifunza. Mwisho niishukuru familia yangu mke na watoto wangu kwa mapenzi mengi yanayofanya kichwa changu kiendelee kutulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, nijibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inachukua hatua zifuatazo ili kukabiliana na hali hiyo: -

(i) Wizara imeaandaa mwongozo wa maadili na utamaduni wa Mtanzania uliozinduliwa Tarehe 02 Julai, 2022 ambao unaendelea kusambazwa;

(ii) Kutoa elimu ya maadili na kufanya uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kwa jamii kupitia Vyombo vya Habari. Mathalani, katika kipindi cha Januari – Aprili, 2023 Wizara imefanya vipindi 11. Pia Maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri 16 kati ya Halmashauri 184 nchini wamefanya vipindi 21 kupitia vyombo vya Habari;

(iii) Kutoa elimu ya maadili kwa wadau wa malezi na makuzi ikiwemo Viongozi wa Dini, wamiliki wa vituo vya malezi na shule za awali na Wasanii. Aidha Wizara inameandaa mdahalo na semina maalum kwa Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakati wa Tamasha la Pili la Kitaifa la Utamaduni litakalofanyika Mkoani Njombe tarehe 19-21 Mei, 2023;

(iv) Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Viongozi wa Dini, Machifu na Viongozi wa Kimila pamoja na Wizara zenye dhamana ya malezi na makuzi ya watoto na vijana pamoja na usimamizi wa maadili nchini katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya pamoja, ahsante.